Juma na mdogo wake Danieli wakiwa wodini
MTOTO ABEBA MAJUKUMU YA FAMILIA
Na Anthony Mayunga
Oktoba 6,2012.
“NILIISHIA darasa la tatu….wadogo
zangu wote hawajaanza shule na sijui kama wataanza ….maana mimi ndiye nimegeuka
mzazi wao…kula kwao ni mimi…wakigua kama huyu mimi ndio wananitegemea ndiyo
maana leo niko wodini nikiuguza mdogo wangu,”ni maneno yaliyojaa simanzi ya
mtoto Juma Deus(12)
Katika mazingira ya kawaida
huwezi kuamini lakini ndivyo alivyokutwa na Mwandishi wa makala hii wodi ya
watoto kitanda namba 1 hospitali teule ya Nyerere ddh wilayani Serengeti mtoto Juma akimuuguza mdogo wake Daniel
Deus(5)akisumbuliwa na malaria na kuishiwa damu.
Anasema alilazimika kutembea
kilometa zaidi ya 25 kwa mguu akiwa amembeba mdogo wake mgongoni kutoka kijiji cha Nyakitono ambako
baba yao Deus Marwa aliwaacha na kwenda kijiji cha Rung’abure baada ya kutoka
hospitali alikokuwa amelazwa na kufanyiwa upasuaji wa tumbo septemba 3 mwaka
huu.
Ilikuwaje?
Anasema septemba 20 majira ya saa
10:00 alfajiri mwaka huu bila kujali giza alilazimika kumbeba mdogo wake baada
ya kuzidiwa na kuanza kutembea huku wakipumzika njiani na kila akipata nguvu
aliendelea na safari.
“Sijui kama watoto wengine
wanapata shida kama zangu,mdogo wangu hakuwa na uwezo wa kutembea nililazimika
kumbeba mgongoni na kila nilipochoka tulikaa chini ,njaa ,uchovu viliniandama
,lakini kila nikikumbuka kama kuwa anahitaji tiba nilipata nguvu na kuanza
safari”anasema huku akilengwa lengwa na machozi.
Anadai alitumia masaa zaidi ya 11
kufika kijiji cha Rung’abure aliko baba yake na kaka yao ambaye ni mtoto wa
baba yao mwingine ambaye ni fundi baiskeli aliyemtaja kwa majina ya Mwita Deus.
“Tulifika tumechoka sana ,njaa na
mdogo wangu kutokana na njaa na ugonjwa hali ilikuwa mbaya,tulimkuta baba akiwa
naye hajapata nafuu ,tukakaa hapo kwa kaka tukawa tunamnunulia dawa mdogo wangu
hali ikawa inazidi kuwa mbaya kila kukicha”anabainisha.
Septemba 27,mwaka huu akalazimika
kuanza safari ya kumpeleka mdogo wake hospitali ya Nyerere ddh kwa kumbeba
mgongoni hadi alipopata msaada kutoka kwa msamaria mwema.
Mtoto huyo ambaye kutokana na
majukumu ya kulea wadogo zake amelazimika kuwa kama mtu mzima anadai alianza safari hiyo lakini akapata msaada
kutoka kwa kaimu afisa mtendaji wa kijiji cha Rung’abure Mkeba Mweri Masiko
akawabeba kwa pikipiki hasa baada ya kumsimulia kilichowakuta.
“Kwa kweli msaada wake sitausahau
kwa kuwa aligeuka kuwa mzazi wetu ,maana hakuishia kutusafirisha tu bali
ameendelea kutusaidia,mpaka sasa ,maana kwa hali aliyokuwa nayo mdogo wangu
tulipofika tu tukalazwa”anadai.
Juma anafafanua kuwa alikuwa na
siku chache tu toka ametoka hospitalini hapo alipokuwa akimuuguza mdogo wake
Wantiko Deus(4)”nimefika nyumbani namkuta huyu naye ana hali mbaya nimekuja
hapa tumelazwa tena ,safari zote mpaka tunatoka hakuna ndugu anakuja kutuona
tunasaidiwa na wagonjwa na ndugu zao wodini,maisha gani haya jamani”anasema kwa
masikitiko.
Licha ya kuwa ni mtoto wa mama
yake wa kambo lakini kwa vile kwao ndiyo mkubwa analazimika kuwasaidia wadogo
zake bila ubaguzi wowote.
Fedha walizopewa kidogo
zilitumika kwa kununua dawa licha ya
kuwa alitakiwa kutibiwa bure kulingana na umri wake lakini aliambiwa hakuna
dawa ,hata hivyo hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu wa dawa kutokana na
kuwa toka Mei hawajapata dawa MSD kwa madai serikali haijatoa fedha za ruzuku.
Fedha hizo pia zilitumika kwa
ajili ya kununulia chakula na zilipokwisha kwa kuwa wamekaa zaidi ya siku tano
huku mdogo wake akitakiwa kula vyakula vizuri na matunda kwa kuwa alikuwa ana
upungufu wa damu ikabidi ategemee msaada wa wagonjwa wenzake.
Maisha yao yalivyokuwa awali.
Mwaka 2009 walikuwa wakiishi
katika kijiji cha Mbalibali baba yao akiwa na wanawake wawili,kisha akahamia
kijiji cha Nyakitono yeye akiwa darasa la tatu walipofika huko hakupelekwa
shule kwa madai kuwa baba yake hana uwezo na baadae mama zao wote wakakimbia na
kuwaacha wao na baba yao.
“Mama yangu Pili Budaga aliondoka
na kwenda kwao Usukumani na mama mdogo Pili Nyamhanga yuko kijiji cha Bonchugu
hao wote waliondoka baada ya kukorofishana na baba ,wakaniachia mzigo huo
najuta kuzaliwa mkubwa maana baba hajali familia yake”anasema kwa uchungu.
Kutojali huko ndiyo maana
hajapelekwa shule yeye na hata wadogo zake waliotakiwa kuanza shule ama
darasa la awali hawajapelekwa,madai ya baba yao yakiwa ni kwamba hana uwezo.
Kutokana na hali ya kifamilia
kuwa ngumu baba yao naye akawa hajali matokeo yake yeye akawa analazimika
kubeba majukumu ya kuwahudumia wadogo zake kwa mahitaji ya chakula na kuchunga
mbuzi walionao.
“Sijui hali ilivyo nyumbani kwa
wadogo zangu kwa sasa wakati mimi niko huku ,wanapataje chakula ,tuna mbuzi 14
nani anawaangalia kwa kweli naumia sana ,sijui hali yao maana Nyamhanga ndiye
mkubwa miaka 10,Wantiko(4)na Rhobi(3)ambao ndio wanaangalia mji”anasema kwa
unyonge.
Muuguzi wa zamu.
Nyamtondo Masini muuguzi wa zamu
wodi la watoto anakiri kuwa hali ya mtoto huyo haikuwa nzuri kwa sababu
walimchelewesha kumfikisha hospitali kwa ajili ya matibabu.
“Mara ya pili mtoto huyu anakuja
na wadogo zake kuwauguza,kwa kweli hili tukio si la kawaida hata kama baba yake
hana uwezo lakini inatakiwa ndugu wasaidie kwa kipind chote anayeonekana ni mtu
aliyewaleta hapa kwa pikipiki baada ya kuwakuta njiani “ anasema.
Shuhuda anena.
Magreth Samweli(32)mkazi wa
kijiji cha Bonchugu ambaye mwanae amelazwa wodi hiyo anasema kwa mara ya kwanza
anashuhudia mtoto anauguza mtoto mwenzake bila hata wazazi ama ndugu kuonekana.
“Huyu mtoto katembea umbali mrefu
akiwa amembeba mdogo wake hadi sasa amefika hospitali hakuna ndugu anakuja
kuwaona badala yake wanaouguza watoto wao humu ndiyo tumegeuka kuwasaidia
“anasema.
Anakichukulia kitendo hicho kuwa
ni cha kinyama na kinakiuka sheria na haki za mtoto kwa kuwa anastahili
kutibiwa na kuhudumiwa na wazazi wake ama ndugu na kutaka serikali iwachukulie
hatua kwa mzazi wake kwa kuwa kitendo cha kuoa wanawake wengi wakati hana uwezo
wa kuwatunza watoto.
Kaimu ofisa mtendaji.
Mkeba Mweri Masiko kaimu ofisa
mtendaji wa kijiji cha Rung’abure anasema baada ya kuwasaidia usafiri hadi
hospitali amelazimika kubeba majukumu ya kuwahudumia baada ya kubaini kuwa
hawakuwa na msaada wowote kutoka kwa ndugu.
“Hata damu nililazimika kutoa
mimi baada ya kuona mtoto huyo anaweza kupoteza maisha,nimegeuka kuwa mzazi wao
maana ninavyozungumza na wewe nimewatoa hospitali wako nyumbani kwangu
nategemea kaka yao akifika niweze kumkabidhi hao wadogo zake,”anasema.
Kaka yake.
Mwita Bhoke ndugu yao na hao
watoto anakiri watoto hao walitembea hadi kijiji hapo wakitafuta msaada baada
ya baba yao kuwaacha na kwenda kupumzika kwake kutokana na ugonjwa aliokuwa
nao.
“Niliondoka kwenda kijiji cha
Mikomarilo Bunda kumwona mgonjwa mtoto huyo akazidiwa ndipo wakampeleka
hospitali,kwa kweli hawakuwa na msaada wowote walijiuguza wenyewe baba yao
alikuwa hapa hana kitu,alichofanya ni kutoka na kwenda kwenda kijiji cha
Bonchugu kumsaka mkewe ambaye ni mama wa watoto hao maana walikuwa
wamekosana”anasema.
Anasema watoto hao wako nyumbani
kwake”hata wale waliobaki kijijini Nyakitono wamekuja huku kwa mguu nan i
wadogo kutokana na kukosa huduma,hapa ninao watoto watatu, Juma ambaye ni
mkubwa ameondoka na wazazi wake kwenda Nyakitono kuangalia mji.”amebainisha.
Akizungumzia uhusiano wao alidai
hao ni watoto wa baba yao mdogo na maisha ya baba yao yamekosa msimamo kwa kuwa
anavurugana na wake zake matokeo yake watoto ndio wana hangaika kama ilivyo
sasa na hata shule imeshindikana.
Matatizo ya watoto yarudisha mahusiano ya wazazi.
Bhoke anafafanua kuwa matatizo
hayo yameweza kurudisha mahusiano ya wazazi kwa kuwa mke wake amerudi ili
waweze kusaidiana kulea watoto ambao wanaleana wao kwa wao huku Juma
akilazimika kubeba majukumu mazito.
Mwenyekiti wa serikali naye avunja kimya.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji
cha Rung’abure Charles Kibure akiongea na Mwananchi Jumapili amesema taarifa za
watoto hao alizipata kupitia kwa kaimu afisa mtendaji na kumsaka Bhoke,hivyo
anataraji kumbana mzazi wa watoto hao ahakikishe anawahudumia.
Kijijini kwake hawana taarifa.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji
cha Nyakitono Juma Porini anasema hana taarifa za familia hiyo ,”huyo Deus
Marwa simjui maana kama kulikuwa na tatizo hilo ,hata hivyo hapa kijijini
tunasaidia wale wasiokuwa na uwezo kabisa kwa matibabu na hata elimu ,ngoja
nafuatilia”anasema.
Wanaharakati.
Baadhi ya wanaharakati wanasema
matukio kama hayo yanachangiwa na wazazi wengi wanaooa wake wengi kutothamini
familia zao na hata kushindwa kuwapeleka shule,lakini hakuna hatua ambazo
wanachukuliwa .
Juhudi za kuwasaka wazazi hao ili
kujua hatima ya watoto hao kwa masuala ya elimu.
Mwisho.0759891849.
0 comments:
Post a Comment