Subscribe:

Ads 468x60px

JANGILI ALIYEKUTWA NA SMG AFUNGWA MIAKA 15 JELA

 ALIYEKUTWA NA BUNDUKI YA KIJESHI,RISASI 96 NA NYARA ZA TAIFA AFUNGWA
MIAKA 15 JELA.
Na Anthony Mayunga-Serengeti
Oktoba 30,2012.

MAHAKAMA ya Hakimu mkazi wa wilaya ya Serengeti imemhukumu  mkazi
mmoja wa kijiji cha Motukeri kata ya Natta wilayani hapa kwenda  jela miaka
15 kwa  makosa ya kukutwa na bunduki ya kivita aina ya smg,risasi 96 na
nyara za taifa.

Aliyekumbwa na adhabu hiyo mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo Franco
Kiswaga ni Sabasaba Nyagekubwa(31) baada ya kukiri makosa yote manne
yaliyokuwa yanamkabili alipofikishwa mahakamani oktoba 29 mwaka huu.

Akitoa hukumu hiyo hakimu Kiswaga alisema mahakama hiyo imemtia
hatiani mtuhumiwa huyo baada ya kukubali makosa manne yaliyokuwa
yanamkabili ikiwemo kula njama za kuingia hifadhini bila kibali.

Makosa mengine ikiwa ni kukutwa na silaha ya kivita aina ya SMG ambaye
kisheria hapaswi kukaa nayo raia ,kukutwa na risasi 96 kinyume cha
sheria na kukutwa na nyara za taifa vipande 10 vya nyama ,mikia 6 ya
nyumbu  na mayai manne ya mbuni.

“Kutokana na makosa hayo ambayo ni kinyume cha sheria na ambayo
yanaonekana kukithiri unahukumiwa kwenda jela miaka 15 ili iwe
fundisho kwa wengine ,kwa kuwa hatujui hiyo silaha kwa muda uliokaa
nayo umeitumiaje”alisema hakimu.

Katika utetezi wake mtuhumiwa aliomba mahakama imuhurumie kwa kuwa ni
kosa lake la kwanza kukaa na bunduki ya kijeshi  na hakuweza kuisumbua
mahakama na ndiyo maana aliposomewa makosa yake alikubali yote.

Mapema  oktoba 29 mwaka huu mwendesha mashitaka mrakibu msaidizi wa
polisi Alfred Marimi aliiambia mahakama kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa
oktoba 25,majira ya saa 11 alfajiri mwaka huu katika kijiji cha
Motukeri alikamatwa akiwa na silaha,risasi na nyara za taifa.

Mbali nay eye watuhumiwa wengine waliokamatwa katika tukio hilo ni
Timoth Omoke(20) mkazi wa Kisii nchini Kenya na Pius Mayenga mkazi wa
kijiji cha Kyandege wilayani Bunda ambaye alikana mashitaka yote na
kurudishwa mahabusu hadi novemba 13,2012 itakapotajwa tena.

Mtuhumiwa baada ya kukubali kosa kesi hiyo iliahirishwa hadi oktoba 30
2012 siku moja kwa ajili ya hukumu,hata hivyo kosa moja la kukutwa na
nyara bado linaendelea  novemba 13  mwaka huu kwa kuwa ni uhujumu uchumi wanasubiri kibali
ili iweze kusikilizwa.
Raia wa Kenya naye ahukumiwa.
Wakati huo huo Omoke raia wa Kisii nchini Kenya aliyekutwa nyumbani
kwa Nyagekubwa amehukumiwa kifungo cha miezi 6 jela ama kulipa faini
ya tsh,250,000= baada ya kubainika kuishi nchini bila kibali.

Omoke ambaye kibali chake kilibainika kuisha toka oktoba 7 mwaka huu
amepelekwa gerezani baada ya kushindwa kulipa kiasi hicho.

Mwisho.

0 comments:

Post a Comment