Subscribe:

Ads 468x60px

Ukeketaji kuanza desemba 15,2012


 wakati tarehe ya kuanza ukeketaji wilayani serengeti ikitajwa kuwa ni desemba 15 mwaka huu siku moja tu baada ya shule za msingi kufungwa wanaharakati wanaendelea na kampeini zao za kupinga vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia,picha kwa hisani ya Mayunga.blogsspot.com
 
UKEKETAJI  KUANZA DESEMBA 15 BAADHI YA MAENEO.
Na Anthony Mayunga-Serengeti
Novemba 28,2012.

WAKATI wanaharakati wanazindua siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ,wazee wa baadhi wa mila baadhi ya maeneo  wilaya ya Serengeti wamepanga kuanza ukeketaji na tohara kwa vijana wa kiume kuanza desemba 15 mwaka huu.

Uamzi wa wazee wa mila kwa baadhi ya maeneo ambao unafanywa kisiri siri imebainika kuwa itakuwa ni siku moja baada ya kufungwa kwa shule za msingi desemba 14,2012.

Habari za uhakika ambazo zimethibitishwa na baadhi ya wazee wa mila zinadai kuwa muda huo umepangwa ukizingatia tarehe ambazo ngariba wa vijana wa kiume atakuwa amemaliza kazi nchini Kenya.

“Ngariba wa kiume anatokea nchini Kenya ambako kwa sasa wanaendelea na kazi ya kutahili…kuanzia tarehe hizo atakuwa amemaliza na ndiyo maana wamepanga tarehe hizo…”alisema  mmoja wa wazee wa mila jina limehifadhiwa.

Aliliambia Mwananchi kuwa ngariba wa kike wapo vijijini lakini kwa mila na desturi  watoto wa kike hawawatangulii vijana wa kiume,hivyo kazi hiyo itafanyika kwa wakati mmoja hasa maeneo ya kata ya Kebancha bancha.

Akizungumzia tishio la serikali la kuwakamata watakaohusika na kukeketa  watoto wa kike ,alisema kuwa kuacha itakuwa kazi ngumu kwa kuwa mila na desturi itakuwa imepotea.

“Ili kutopoteza mila wanakata kidogo sana ili damu ionekane imevuja,kuacha kabisa ni vigumu haya mambo yatakwenda taratibu yaishe yenyewe kama ilivyokuwa kwa kutoga masikio”alibainisha.

Hata hivyo baadhi ya maeneo wazee wa  mila wakiulizwa msimamo wao kuhusu kuacha ukeketaji wamekuwa wakisukumia wanawake kuwa ndio wanashawishi watoto wa kike ,huku akina mama wakisema wenye sauti ni wazee wa mila kwa kuwa ndio wanaoheshimiwa na jamii.

“Kuna kusukumiana kwa wazee wa mila na akina mama … wazee wa mila wanasema akina mama wanachangia kuendelea kwa ukeketaji kwa kuwa huwadanganya watoto kuwa wanaenda kusalimia bibi zao …huko hukeketwa kwa aibu yao kwa jamii ni kubwa kuliko wanaume,”alisema.

Kwa mjibu wa tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa wanawake wananyanyapaliana sana kama  kuliko wanaume hasa mabinti zao wanapokuwa hawajakeketwa,hali ambayo pia huwaathiri watoto wa kike kutengwa na wenzao na wengine hutoroka kwenda kukeketwa.

Baadhi ya mashirika yanayotoa  elimu ya kupinga vitendo vya ukeketaji  kwa wilaya za Serengeti na Tarime hasa Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT)wamesema kuwa wana uhakika wa kupokea watoto wengi watakao kimbia kukeketwa.

Mwisho.


BABA ABAKA MWANAE WA MIAKA 2.5 NA KUMUUMIZA VIBAYA.
Na Anthony Mayunga-Serengeti
Novemba 28,2012.

WAKATI wanaharakati wakipaza sauti za siku 16 za kupinga ukatili ,mkazi mmoja wa mtaa wa Sedeko kata ya Stendi kuu wilayani Serengeti John Nashon(25)amembaka mwanae wa miaka 2.5 na kumuumiza vibaya kisha akatoroka.

Tukio hilo ambalo limepokelewa kwa hisia tofauti na wakazi wa mji wa Mugumu linadaiwa kutokea novemba 26,majira ya saa 12.00 jioni mwaka huu katika mtaa huo na kuripotiwa kituo cha polisi Mugumu mjini.

Mama mzazi wa mtoto huyo akiongea na Mwananchi akiwa hospitali teule ya Nyerere ddh alikolazwa kitanda namba 8 wodi ya watoto ,alisema wakati unyama huo unatendeka alikuwa sokoni.

“Nilimwacha mwanangu na baba yake ambaye ni fundi wa magari gereji ya Mayala mjini hapa,kurudi kufika mlangoni mme wangu akanieleza niingie ndani haraka nimkande mtoto mwili mzima kwa maji baridi…nilikuwa sijui kinachoendelea”alisema na kuendelea

“Kuingia chumba cha kulala nikamkuta mtoto amelala kitandani,kumnyanyua damu zikamwagika mithili ya maji kutoka sehemu yake ya siri…kumwangalia nikakuta amechanika sehemu zake za siri”alisema.

Hali hiyo ilimpelekea kumwangukia mwanae na kuanza kulia kwa uchungu na alipotaka maelezo kwa mme wake alisema alimsukuma kwa bahati mbaya mwanae akaanguka kwenye kochi na kuchomwa na msumari sehemu zake za siri.

“Nilipomwambia tumpeleke hospitali akakataa tena akinitishia kunipiga kwa madai kuwa siri itafichuka…niligundua kumbe ndiye kafanya unyama huo,nilitoka kwa nguvu hadi kituo cha polisi na kupewa pf 3,nikimwacha hapo,lakini alikimbia na haijulikani alipo”alisema.

Hata hivyo alipomuuliza mwanae kilichomtokea akasema kuwa baba yake ndiye aliyemfanyia unyama,huku akishangaa kwa kitendo hicho kwenye ndoa yao iliyodumu kwa mwaka mmoja toka novemba 2011.

Mganga mkuu wa hospitali hiyo Dk.Kelvin Mwasha amekiri kumpokea mtoto huyo na kuwa amelazwa wodi la watoto ,kutokana na maumivu na kuvuja damu nyingi ililazimu kuongezewa damu.

“Sehemu zake za siri zilikutwa zimeharibiwa sana ,amepata huduma ikiwa ni pamoja na kuchukua sampuli za maji yaliyokuwa yanatoka ukeni kwa ajili ya vipimo …amekutwa yuko salama,lakini hili tukio si la kawaida linatakiwa kulaaniwa ,na ndiyo yanaifanya wilaya kuonekana na matukio ya ukatili”alisema.

Hivi karibuni katika uzinduzi wa siku 16 zakupinga ukatili kamanda wa polisi mkoa wa Mara Absalom Mwakyoma alisema kunaongezeko kubwa la matukio ya ukatili,ambapo kwa mwaka huu toka januari yameripotiwa matukio 201 ikiwa ni tofauti na mwaka 2011 matukio 148 yaliriripotiwa polisi.

Mwisho.

0 comments:

Post a Comment