POLISI NYAMONGO
WADAIWA KUUA KWA RISASI
Na Anthony
Mayunga-Mara
Novemba 6,2012.
ASKARI polisi wa mkoa wa kipolisi Tarime na Rorya wanadaiwa
kumuua mkazi mmoja wa kitongoji cha Nyabegena kijiji cha Kewanja wilayani
Tarime kwa kumpiga risasi baada ya kutokoea vurugu wakati wanawatawanya
wananchi waliokuwa wamepata mchanga unaodaiwa kuwa na dhahabu.
Tukio hilo
linadaiwa kutokea novemba 6 majira ya saa 9.10 arasili mwaka huu katika eneo la Nyabegena kuliko na mgodi Gokona wa kampuni ya African Barrick North
Mara .
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Tanzania O’mtima
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo
na kumtaja aliyeuawa kuwa ni Kibwabwa Ghati Marembera mwenye umri katii ya
miaka 22-25 mkazi wa kijiji hicho ambaye alipigwa risasi na kufumua fuvu la kichwa
na ubongo kumwagika.
“Ni kweli amekufa mimi nilikuwa kwenye kikao ofisini
sikuwepo eneo la tukio sijajua ilivyokuwa,…lakini kuna taarifa kuwa watu walikuwa wanataka
kuingia mgodini kuchukua mawe ya dhahabu…risasi zimepigwa nyingi sana na eneo hilo
ni karibu na makazi ya watu”alisema.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio akiongea na Mwananchi kwa njia
ya simu anasema kuwa polisi walikuta wananchi wana mawe yanayodaiwa kuwa ya
dhahabu waliyoyapata kwenye vifusi na kutaka kuwanyanganya ndipo vurugu
zikaanza.
“Polisi wamezoea kuwanyanganya wananchi mawe ya dhahabu na
kujimilikisha,yalifika magari kama matano ya polisi na kuanza kuwazingira kwa
lengo la kuwapora ndipo vurugu zikaanza,wananchi wakipinga ,wamepiga risasi
nyingi sana ndipo wakawapiga risasi watu wawili mmoja ni Marembera aliyekufa
hapo hapo na mwingine hatujajua jina lake amepigwa ubavuni”alisema shuhuda.
Na kuwa baada ya kuwa wamewapiga risasi vurugu zimeendelea
huku polisi wakitaka kuchukua mwili wake waondoke nao lakini wamezidiwa na
wananchi na kufanikiwa kuchukua majeruhi mmoja na kukimbia kwenda Tarime.
“Polisi wamezidiwa na wananchi wakashindwa kuchukua mwili wa
marehemu kuondoka nao,lakini majeruhi ambaye hajafahamika wamemchukua ,kwa hali
aliyokuwa nayo sidhani kama atapona”anasema.
Alibainisha kuwa mwili wa marehemu huyo umepelekwa kituo cha
afya cha Nyangoto maarufu kama sungusungu kwa
ajili ya kuhifadhiwa na uchunguzi zaidi.
Mmoja wa waganga katika kituo hicho cha afya aliyefahamika
kwa jina moja la Kenedy alipoulizwa na Mwananchi kwa njia ya simu kama wamepokea mwili wa Marembera ama kuwepo majeruhi
wengine alidai kuwa yeye alitoka kazini mapema hivyo hajui.
Hata hivyo alipoulizwa kama
tukio limetokea kabla ya muda wa kazi haujasha imekuwaje atoke muda mrefu na
hakurudi kazini ,alidai,”mimi nakwambia nimetoka muda mrefu sijui na wala sijui
nani yupo zamu”alijibu.
Kamanda wa polisi wa mkoa huo wa kipolisi Justus Kamugisha
alipoulizwa kwa njia ya simu alidai,” taarifa nilizopata ni kwamba kuna vurugu
zimetokea za watu kuvamia mgodi na mmoja nasikia ameumizwa haijulikani yuko
wapi,nafuatilia habari kamili nitatoa baadae”alisema.
Huo ni mwendelezo wa matukio ya askari polisi wa kanda hiyo
kuua raia katika mgodi huo ,inadaiwa sababu kubwa ni serikali kutokutenga
maeneo ya wachimbaji wadogo wadogo.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment