Subscribe:

Ads 468x60px

Njaa yawatesa wakazi wa Ngorongoro


SERIKALI YALAUMIWA KWA KUTOPELEKA CHAKULA NGORONGORO LICHA YA KULIPWA.
Na Anthony Mayunga-Ngorongoro
November 18,2012.

SERIKALI imeombwa kuchukua za hatari kupeleka chakula kwa wakazi wa kata 7 zilizoko tarafa ya Ngorongoro wilayani Ngorongoro wanaokabiliwa na baa la njaa.

Wakazi wa tarafa hiyo iliyo ndani ya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro hawaruhusiwi kulima kwa kuwa eneo hilo limehifadhiwa,na wanategemea shughuli za ufugaji ambazo zinakabiliwa na tatizo kubwa la ukame.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Elias Ngorika ameliambia Mwananchi kuwa hali ya chakula ni mbaya sana hali ambayo inatishia maisha ya wakazi wa tarafa hiyo kama juhudi za haraka hazitachukuliwa.

“Hali ni mbaya maana kilio hiki tumeishaiambia serikali inatakiwa kuzinduka… chakula kiliagizwa kwenye ghala la akiba ya chakula toka agosti fedha zimelipwa… hawajaleta,serikali isisubiri watu wafe ndipo izinduke “alisema kwa unyonge.

Alisema kiasi cha tsh,mil,315 zilizotokana na fedha zinazotolewa na mamlaka ya hifadhi ya Ngoro ngoro kwa baraza la wafugaji zimeishalipwa kwa ajili ya kupata tani 190 ,”chakula hicho kingepatikana hali ingekuwa nafuu”alisema.

Hata hivyo alisema kwa watu wazima kusubiri kupewa chakula kila wakati ni tatizo hivyo kungeangaliwa mfumo mwingine wa kuziwesha kiuchumi  familia zinazoishi ndani ya eneo hilo lililohifadhiwa .

Alisema baraza la madiwani katika kikao chacha hivi karibu waliamua kumwona Rais Jakaya Kikwete Arusha kumpelekea kilio cha wananchi ,lakini walizuia kukutana naye na kulazimika kukutana na mkuu wa mkoa.

“Kwa sasa suala hilo tumeliwekea mkakati wa kimkoa ili kuhakikisha tunawanusuru na vifo na magonjwa ya utapiamlo… hili suala lina uzito wake kwa kuwa wananchi hawatakuwa rafiki wa uhifadhi ili tusifike hatua mbaya wasaidiwe”alibainisha  Ngorika.

Mkakati wa kwanza kwa sasa wameunda kikundi maalum kinachoshirikisha wataalam ngazi ya mkoa ,wilaya na baadhi ya madiwani ili kujua ukubwa wa tatizo na taarifa itatoka ndani ya muda mfupi.

Kata ambazo zinakabiliwa na njaa ni Kakesio,Orbal orbal,Ngorongoro,Endulen,Nainokenoke,Naiyobi na Kapenjoro.

Afisa utawala baraza la wafugaji Ngorongoro Nakuroy Parkepu alisema serikali inatakiwa kuchukua hatua za kuwapa wananchi chakula kwa kuwa toka baraza limeagiza ni miezi mitatu lakini serikali haijawafikishia chakula.

“Hili ni tatizo la serikali sisi tumelipa toka agosti hawajaleta chakula wananchi wanahali mbaya …huu ni udhaifu wa serikali na vyombo vyake…hatuwezi kukiuka sheria za manunuzi “amebainisha.

Amekiri kuwa kila mwaka wa fedha mamlaka ya fifadhi Ngorongoro inatoa zaidi ya tsh,bil 1 kwa baraza kwa ajili ya shughuli za maendeleo,lakini zaidi ya tsh,mil 400 huelekezwa kwenye elimu,bado ujenzi wa sekondari ,afya ,maji na huduma zingine .

“Fedha hizo si za kununulia chakula,bali ni za huduma ya jamii,inapotokea tatizo kama hilo tunatoa hapo hapo ni kiasi kidogo”alidai.

Bei ya mahindi kwa sasa gunia moja ni tsh,78,000= ambayo wanategemea kutoka Karatu ambako kwa sasa debe ni tsh,12,000= kabla ya kusafirisha.

Makamu wa Rais wa jukwaa la Wanataaluma na Sauti ya Jamii wilayani Ngorongoro Onesmo Ole Ngurumwa akiongea na mwananchi kwa njia ya simu amesema serikali isikwepe lawama matatizo ya njaa kwa wakazi wa tarafa hiyo kwa kuwa imeshindwa kupeleka chakula kwa wakati.

“Jukwaa limeitisha kikao novemba 24 mwaka huu ili kuzungumzia hali hiyo na mengine ikiwemo mapigano,lakini haiwezekani watu waishi kwa chakula cha msaada  kila mwaka… huu ni udhaifu wa viongozi kufikiri”alibainisha.

Alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa wilaya hiyo ni tajiri  ambayo inaingizia taifa takriban zaidi ya bilioni 50 kwa utalii ,wananchi wanaendelea kutaabika kwa kuishi maisha mabaya zaidinya wanyama .

Mwisho.

0 comments:

Post a Comment