Subscribe:

Ads 468x60px

Mamlaka ya mji mdogo wa Mugumu yadaiwa kutiririsha kinyesi kwenye makazi ya wananchi



MAMLAKAYA MJI MDOGO YALAUMIWA KWA KUTIRIRISHA MAJI MACHAFU KWENYE MAKAZI YA WATU NA SEHEMU ZA BIASHARA.
Na Anthony Mayunga-Serengeti.
Novemba 8,2012.

MAMLAKA ya mji Mdogo wa Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara imelalamikiwa kwa kushindwa kudhibiti mfumo wa maji machafu ynayotoka choo cha soko hilo na kutiririkia kwenye maeneo ya nje ya soko ambako ni makazi ya wananchi wa mtaa wa Sedeco.

Mbali na kutiririsha maji machafu kwenda kwenye makazi ya wananchi,pia choo hicho hakina maji hali ambayo inawalazimu watoa huduma kusomba maji kwa ndoo,huku harufu kali inayotoka ndani ya vyoo hivyo kutokana na ukosefu wa maji ya kutosha inaathiri wafanyabiashara ndani ya soko.

Soko hilo ambalo linategemewa na wakazi wa mji huo  na viunga vyake ikiwemo hoteli na kambi nyingi za kitalii zilizomo ndani na nje ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti lilijengwa kwa msaada wa shirika la misaada la Sweden(SIDA).

Pamoja na kilio cha wananchi  wanaoathiriwa na maji hayo yanayovuja kwa wingi kutokana na bomba kupasuka bila kusikilizwa na watendaji ,  walilazimika kuwasilisha malalamiko yake kwa  mbunge wa jimbo hilo Dk,Stephen Kebwe ambaye  alitaka kujua kama hawana fedha na kuthibitishiwa kuwa fedha si tatizo.

Hata hivyo Mwananchi ilibaini kuwa toka  oktoba hakuna utekelezaji wowote uliofanyika na hali inazidi kuwa mbaya zaidi huku baadhi ya wafanyabiashara walioko maeneo jilani na choo na kule maji yanakovuja wakilalama kukosa wateja.

Phinias Edward mfanyabiashara eneo la sedeko nje ya soko amesema bomba hilo la maji machafu limepasuka kwa muda mrefu na hakuna hatua zinazochukuliwa zaidi ya wahusika hasa maafisa afya kushughulikia wafanya biashara ndogo ndogo kuwa wanafanyia kazi mazingira machafu.

“Mimi nauza chakula hapa wateja hawaji kwa sababu bomba la maji machafu ya kinyesi limepasuka,harufu na nzi inatishia uhai wetu,maafisa afya wanatujibu kijeuri kuwa kutokana na harufu hiyo matumbo yanajaa hatutakula sana..,majibu yanaonyesha dharau kwa wananchi na kushindwa kufanya kazi zao”alisema.

Mmoja wa wafanya biashara ndani ya soko jina limehifadhiwa alisema kwa sasa hali yake kiuchumi ni mbaya sana kwa kuwa amepoteza wateja wake kutokana na harufu inayotoka kwenye choo hicho kwa kuwa kimejengwa bila kuwepo bomba la kutolea harufu mbaya nje ,na kulazimika kutolea kwenye mashimo(chemba).

“Jilani yangu amefunga duka kutokana na hali hiyo,watalaam wa mamlaka kila kukicha wanakuja kupima wanaondoka,maji hayatoki bombani hata vyakula ,matunda hayaoshwi,maji yamebaki ya kusomba kwa mtu wakati mji mzima una bomba”alisema.

Alisema waliomba choo kifungwe kwanza ili kitengenezwe wakakataa ,uamzi ambao unaonekana kuwanufaisha watendaji wanaopata fedha kupitia kwa mtu waliyembinafishia choo na bafu wakati ni chafu.

Mmoja wa watoa huduma katika choo na bafu alisema kuwa wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji kwa kuwa choo hakina mfumo wa bomba ,na wateja wake wanalalamika na wanakabiliwa na harufu mbaya licha ya kuweka dawa kwa kuwa mfumo wa kutoa hewa haupo na inashindikana kupumua kwa nje hewa chafu inapitia chemba zilizopo sokoni.

Tatizo lilifikishwa baraza la madiwani.

Tatizo hilo pia liliwasilishwa katika baraza la madiwani wa halmashauri hiyo ambao waliagiza bomba la maji machafu lililobomoka liwe limefanyiwa ukarabati haraka kabla ya septemba 21,mwaka huu.

Baraza la madiwani ladanganywa.

Katika taarifa ya utekelezaji katika  baraza hilo lililoketi oktoba 31 mwaka huu ilisomwa kuwa “azimio limetekelezwa,matengenezo ya kutengeneza bomba lililokuwa limepasuka na kutoa maji machafu limefanyiwa marekebisho”mwisho wa nukuu ya majibu.

Hakuna matengenezo yoyote yaliyofanyika na maji yaliyochanganyika na kinyesi yanavuja katika makazi na sehemu za biashara za mama ntilie na wauza mkaa,huku watendaji wakikwepa kuzungumza.

Ofisa afya wa Mamlaka ya mji mdogo Chironge Hamisi alitafutwa ofisini kwake hakuweza kupatikana ,lakini alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi alidai yuko nje ya ofisi ,huku akikwepa kuzungumzia tatizo hilo.

“Suala la maji machafu kwanini leo hii ndipo wananchi wanalalamika ,wakati mji hauna maji hawakulalamika, leo sirudi ofisini labda kesho ili tuzungumze kuhusu tatizo hilo,wamefikaje kwako”alisema na kukata simu.

Ofisa mtendaji wa mji ndogo Obel alipotafutwa ofisini kwake hakuweza kupatikana ,kupitia simu yake ya mkononi alidai yuko bomani kikazi nakuomba atafutwe ofisa afya ndiye mwenye maelezo,hata hivyo alipoambiwa amegoma kulisema akadai ataongea.

“Wewe mtafute ataongea tu ndiye ana maelezo ya tatizo hilo,mimi niko nje ya ofisi”alisema.

Baadhi ya wenyeviti wa vitongoji walioko kwenye kamati ya huduma za jamii walisema suala hilo wamelipigia kelele lakini hakuna utekelezaji wowote.

Mwisho.

0 comments:

Post a Comment