BOMBA LILILOKUWA LIKITIRIRISHA MAJI MACHAFU
YALIYOCHANGANYIKA NA KINYESI LAZIBWA.
Na Anthony Mayunga-Serengeti
Novemba 19,2012.
HATIMAYE mamlaka ya mji mdogo
wa Mugumu wilayani Serengeti umeziba bomba lililokuwa likitiririsha maji
machafu yaliyochanganyika na kinyesi kwenda kwenye makazi wa watu na sehemu za
biashara mtaa wa sedeko.
Uzibaji wa bomba hilo umekuja
siku chache tu baada ya gazeti la Mwananchi kuripoti tukio hilo ambalo
limepigiwa kelele ikiwa ni pamoja na kuwasilishwa katika vikao vya baraza la
madiwani bila ufumbuzi.
Baadhi ya wakazi wa mtaa wa
Sedeco waliliambia gazeti hili kuwa siku moja baada ya taarifa kutolewa
hukuikionyesha picha ya tatizo hatua ilichukuliwa haraka .
“Tunawashukuru sana waandishi
wa habari maana tumeumia sana kwa muda mrefu,mbunge amekuja mara mbili kapuuzwa
,baraza la madiwani lilidanganywa lakini mmekuja hapa na kuandika na hatua
zikachukuliwa huku wakilaumu kwa nini tunawaambia waandishi,watendaji hawa
hawafai mpaka wasukumwe”alisema mmoja akina mama ntilie eneo hilo jina
limehifadhiwa.
Hata hivyo wakazi wa mtaa huo
na wafanyabiashara walimtupia lawama afisa afya wa mamlaka hiyo kuwa utendaji
kazi wake ni mbaya kwa kuwa wanapompelekea malalamiko anawajibu vibaya.
“Hatujui nafasi hizi
wanazipataje maana ofisa afya wa mamlaka hii hafai bomba liko mita kumi toka
ofisi yake ,tunamweleza anatujibu kuwa ,harufu hiyo inawapunguzia bajeti ya
kula kwa kuwa matumbo yatashida yamejaa,tutegemee nini kwa mtumishi kama huyo
analipwa kwa kazi gani”alihoji Phinias Edward mfanyabiashara wa chakula eneo
hilo.
Hata hivyo alipotafutwa kwa
njia ya simu afisa afya huyo Chironge Hamisi kutaka kujua utekelezaji wa kazi
hiyo na malalamiko ya wananchi aling’aka.
“Wewe walikuletea malalamiko
ili tutengeneze hilo bomba,kwanza wewe unaniuliza hayo wewe ni mkuu wangu wa
kazi,mbona unaniuliza uliza haya mambo unataka nini,wewe nini bwana”alijibu kwa
ukali na kukata simu.
Hata hivyo ofisa mtendaji wa
mamlaka hiyo Gidioni Obel alidai kuwa matatizo yote hayo yanashughulikiwa kwa
awamu na kuwa suala la bomba wamemaliza ,lakini ukarabati wa choo ikiwa ni
pamoja na kuweka mifumo ya maji kwa kuwa ilijengwa vibaya inahitaji bajeti
kubwa na wakipata fedha wataitekeleza.
Malalamiko ya wananchi
wakiwemo wafanyabiashara ndani ya soko yalikuwa ni utiririshaji wa maji machafu
yaliyochanganyika na kinyesi kwenye maeneo yao,huku baadhi ya wafanyabiashara
wakilalamikia harufu mbaya inayotokana na choo
hicho kutokuwa na mfumo wa kutolea hewa na maji .
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment