NGARIBA ANASWA BAADA YA
KUWAKEKETA WATOTO WAWILI.
Na Anthony Mayunga-Musoma
Novemba 15,2012.
NGARIBA na mmoja wa wazazi
wakazi wa kijiji cha Masurura kata ya Bwiregi wilaya ya Butiama wanashikiliwa
na jeshi la polisi mkoa wa Mara kwa tuhuma za kuwakeketa watoto wawili wa kike
ambao ni wanafunzi wa shule ya msingi Masurura.
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao
novemba 10 mwaka huu kunakuja huku
maeneo mengi maandalizi ya kuwakeketa watoto wa kike yanaendelea ,wakisubiri shule za msingi zikifungwa.
Kamanda wa polisi mkoa wa
Mara Absalom Mwakyoma amewataja walikamatwa kuwa ni ngariba Bhoke
Wambura(60)mkazi wa kijijini hapo ambaye anadaiwa kuwakeketa watoto wawili na
mmoja kufanikiwa kukimbia na kujisalimisha polisi.
Amesema ngariba huyo alilipwa
tsh,5,000 na kuwakeketa watoto wawili ambao majina yake yamehifadhiwa na ikiwa
ni kinyume na sheria ya makosa ya kujamiiana ya mwaka 1998 na sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.
“Pamoja na ngariba
tumemkamata mama ya mmoja wa watoto waliokeketwa Ghati Mwita(48)wote wa
kijijini hapo ,tunawashikilia na tutawafikisha mahakamani kwa kosa hilo wakati
wowote”alisema.
Kamanda huyo alisema mtoto
aliyetoroka kwa kukwepa kukeketwa na kujisalimisha polisi wamemhifadhi kituo
cha polisi Musoma wakiendelea kuwasaka wote waliohusika katika mpango huo
unakiuka sheria na Haki za Binadamu.
Kutokana na maandalizi
yanavyoshika kasi tayari ameelekeza nguvu katika kata za Ryamisanga,Wegero na
Kamugendi kwa wilaya ya Butiama ambako inadaiwa kuwepo maandalizi ya ukeketaji.
“Nimeishatoa maelekezo kwa
kila kamanda wa polisi wa wilaya kuhakikisha maeneo yote yanayodaiwa kuwepo
maandalizi yafuatiliwe ili watakaohusika wakamatwe kwa kuwa hatuwezi kuona
sheria zinavunjwa ,maana hayo ni makosa ya jinai”alisisitiza kamanda.
Hivi karibuni mkuu wa mkoa wa
Mara John Tupa akiongea naBlogu hii kwa njia ya simu kuhusiana na mikakati ya
mkoa kukabiliana na ukeketaji alisema viongozi wote kuanzia ngazi za vitongoji
,wazee wa mila wameishaelezwa msimamo wa serikali.
Alisema atakayekaidi
atakamatwa na kushitakiwa kwa mjibu wa sheria na kuwaomba wazazi na walezi
kuhakikisha wanatii bila shuruti kwa kuwa hawatasita kuwafikisha mahakamani.
Shirika la Chidren’s
Dignity Forum(CDF) lililoko wilayani Tarime likizindua ripoti ya utafiti lilisema kuwa watoto 4,000
wilayani Tarime wako hatarini kukeketwa.
Pamoja na msimamo wa serikali
kumebainika kuwepo mbinu mbalimbali zinazoandaliwa na wazee wa mila kuhakikisha
watoto wa kike wanakeketwa ikiwemo kazi hiyo huenda ikafanyika usiku,kwa walio
mipakani kupelekwa nchi Kenya kwa ajili ya kukeketwa .
Pia baadhi ya vijana kutishia
kugoma kutahiriwa iwapo wasichana hawatakeketwa kwa kuwa hukaa jandoni wote na
hutoka siku moja,msukumo ambao unawapelekea wazee wa mila kuhaha kuhakikisha
ukeketaji unafanyika ili kulinda mila na desturi.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment