Subscribe:

Ads 468x60px

familia ya watu 16 haina makazi wanalala chini ya mti







 Bhoke Samsoni(19)akiwa na mwanae wa mwezi mmoja ,analazimika kulala humo mvua ,jua lao baada ya nyumba zao kuchomwa moto na wananchi maarufu kama ritongo baada ya kumtuhumu mme wakeWegesa Mwita Sungura(23)kwa wizi wa sola(picha na Anthony Mayunga





FAMILIA YA WATU 16 HAINA MAKAZI,WANALALA CHINI YA MTI.

“nyumba zimechomwa moto,mashamba yameuzwa,hawaruhusiwi kwenda kwa mtu
wala kutembelewa,kisa mmoja atuhumiwa kuiba sola ya zahanati”.
Na Anthony Mayunga
Novemba 2,2012.

“JUA,mvua…baridi vyote vyetu pamoja na watoto hawa wadogo hasa huyu
wangu wa mwezi mmoja…nyumba na mali zetu zimechomwa moto…kana kwamba
haitoshi wamepiga marufuku kwenda kwa jilani na jilani kuja
kwetu…hatuna msaada jamani bora wangetuua kuliko mateso makali kama
haya..”anasema Bhoke Samson(19) mkazi wa Mbalibali wilayani Serengeti.

Mwanamke huyo ni miongoni mwa familia ya watu 16 wa kitongoji cha
Kwirango kijiji cha Mbalibali,kata ya Mbalibali wilayani Serengeti
mkoa wa Mara wasiokuwa na makazi kufuatia uamzi wa kikao cha
jamii(Ritongo)chini ya wazee wa mila kuwachomea nyumba.

Uchomaji wa nyumba zao 8 ulifanywa mchana kweupe bila kujali madhara
wanayopata wakiwemo watoto wadogo ambao baadhi sasa hawaendi shule na
kuwaacha wakilala chini ya miti kipindi hiki cha mvua za masika.

Uamzi ambao ni ukiukwaji wa Haki za Binadamu na ambao unaufanya mkoa
wa Mara kuhesabiwa kati ya mikoa inayoongoza kwa ukatili,unafanywa na
vyombo visivyokuwa vya kisheria (ritongo)ambavyo vimepewa uhuru mkubwa
na watendaji wa serikali.

Kisa cha unyama huo.
Bhoke anadai oktoba 26 majira ya saa 10 jioni mwaka huu kundi la watu
zaidi ya 200 wakiwa na silaha mbalimbali za jadi walivamia mji wao
wakidai wanawachomea nyumba kwa madai  kuwa mme wake Wegesa Mwita
Sungura(23)anatuhumiwa kwa wizi wa sola ya zahanati.

“Toka agosti mwaka huu wanatafuta mwizi wa sola hiyo hakuna mtu
amewahi kujitokeza kueleza kama walimwona ,wamezunguka bila mafanikio
lakini kupitia ritongo linaloongozwa na wazee wa mila wakaamua kuja
kuchoma nyumba zote”anasema kwa huzuni.

Akiongea kwa vituo kutokana na uchungu alionao anadai waliamu
kuwachomea nyumba ,wameteketeza chakula ,vitu vichache walifanikiwa
kuokoa,”inauma sana…bora usishuhudie unyama kama huo maana kama mme
wangu ana makosa iweje wasimkamate…tunaadhibiwa sisi hadi huyu mtoto
wa mwezi mmoja kweli…utawala wa sheria uko wapi jamani…”anasema huku
akifuta machozi.

Anabainisha kuwa mji huo ni shemeji yake Daniel Mwita Sungura ambaye
yeye na familia yake ikiwemo mama mkwe wake wameathiriwa na adhabu
hiyo na hata mashamba yao yameuzwa na wazee wa mila kwa maana wahame
eneo hilo.

Adhabu ya pili eneo lao lauzwa.

“Tukiwa bado tunajiuliza sababu ya kutendewa unyama huo kwa kosa
ambalo hatuhusiki,wazee wa mila waliongoza uuzaji wa mashamba yyetu
yote ikiwemo na chakula …wanapewa ng’ombe na pesa na watu wanapanda
mikonge…hapa tulipo tuko maeneo ya watu …kwa kweli hakuna wakati
tunaohitaji msaada kama sasa…”anasema Bhoke.

Anadai siku ya kwanza walipata msaada kutoka kwa majilani na ndugu
wakajistiri na watoto wao lakini sasa hawana namna zaidi ya kukaa eneo
hilo baada ya kuamriwa wasiingie mji wa mtu wala kutembelewa.

Rhobi Daniel(20) mke wa Sungura ambaye ni mjamzito anayeweza
kujifungua wakati wowote anasema hajui hatima yake kama akishikwa na
uchungu hapo wanapolala kwa kuwa si sehemu salama,huenda akapata
matatizo wakati wa kujifungua.

Alilazimishwa kumchomea mdogo wake nyumba akakataa wakachoma zake.

Daniel Mwita Sungura(33)ambaye ndiye mwenye mji anadai kundi hilo
lilipofika kufanya unyama huo aliwaambia wamchukue mtuhumiwa wampeleke
polisi kwa kuwa pale ni kwake yeye anaishi naye kama mdogo wake na
mama yao mzazi.

“Walikataa na viongozi wa mila wakaniamuru mimi nichome nyumba mbili
za mdogo wangu anazoishi na wake zake wawili…nilikataa kutekeleza
unyama huo tena kwa mdogo wangu…nikawaambia kama wana uhakika ni mwizi
anaeneo lake la ardhi wauze walipe hiyo sola…walikataa ndipo wakaamua
kuteketeza nyumba zote”anasema kwa masikitiko.

Adhabu ya tatu kubwa watupiwa mawe kama ishara ya laana.

Anadai kuwa oktoba 30 majira ya saa 8 alasiri kundi la watu zaidi ya
200 likiongozwa na wazee wa mila walifika eneo lao wakiwa na
fimbo,marungu na mawe  na kuwarushia laana ikiwa ni hitimisho la
adhabu kubwa kwao .

“Wanawake walivua nguo na kuinamia eneo letu…wanaume wakiwa
wanatutupia mawe kinyume nyume kisha wakaondoka ,hiyo ikiwa ni ishara
kuwa hatutakiwi kuingia mji wa mtu wala mtu kuingia kwetu atakayefanya
hivyo atachomewa nyumba”anasema .

Uamzi huo ukiwa unakiuka maagizo ya kamati ya ulinzi na usalama ambayo
iliagiza wajengewe nyumba mbili kwa haraka ,baada ya kukosekana
ushahidi kuwa wanayemtuhumu alihusika na tukio hilo.

“Kitendo hicho kimezidi kutuumiza kwa kuwa hata ndugu zetu hawawezi
kufika kutuona…ninashangaa sana kama wazee wa mila walioaminika ndani
ya jamii wanaongoza vitendo vya ukatili namna hii na kueneza chuki
ndani ya jamii…uamzi huo una agenda nyuma yake”anasema.

Wazee wa mila walikataa kwenda kuwapeleka kula amini.

Anabainisha baada ya kutafuta bila mafanikio aliwataka wazee wa mila
wakubali mdogo wake apelekwe kula amini ambayo inaaminika kama hatua
ya mwisho kwa jamii ya wakurya,lakini walikataa bila kumpa sababu.

“Amini(Kehore)ni hatua ya mwisho kwa jamii yetu maana hupewa maji
yaliyochanganywa na dawa ndani ya fuvu la mtu ,anayekula huapiza kama
ametenda ateketee na familia yake,na hukutwa na majanga kama
amehusika,lakini walikataa badala yake wakakimbilia kukamata ng’ombe
wake 22”anafafanua.

Hata hivyo baada ya kufuatilia oktoba 12 mwaka huu alirudishiwa
ng’ombe wake lakini wakiapa kuwa lazima wawakomeshe ,ndipo
wakawafanyia unyama huo ukienda sambamba na kuuza mashamba yao ekari
70 baadhi yakiwemo mazao.

Vitu vilivyoungulia ndani.

Vitu vilivyoungua ikiwemo nyumba  8 ikiwemo mazao(mtama zaidi ya
magunia 20 aliyokua ananunua kwa ajili ya kuuza  na vitu vinginevyo na
fedha zake  vina jumla ya ths,10,640,000=.

Pia baadhi ya mifugo yake imepotea huku baadhi ya kuku wakidaiwa
kuungulia ndani na wengine kuporwa na wananchi hao.

Wanavyolala.
Familia hiyo inatumia maghala ya kuhifadhiia chakula kama nyumba huku
mifuniko yake ikitumika kukinga kwa juu,hata hivyo ni wachache
wanaopata nafasi humo wengi hujibanza chini ya mti.

Mtuhumiwa.

Wegesa Mwita Sungura(23)kwa masikitiko anasema tuhuma zote
anazohusishwa za wizi ni za kutunga kwa kuwa hata waliokamatwa
wakituhumiwa wa kijiji cha Merenga hawakuwahi kumtaja.

“Toka mwezi wa nane wanadai nimeiba tumekaa vikao vya ritongo zaidi ya
mara tatu hapakuwahi kutokea mtu wa kunitaja,lakini tukitoka wanasema
watanikomesha,wapo waliokamatwa kwa tuhuma hizo mbele ya kikao cha
mila cha vijiji viwili hawakunitaja… iweje leo watufanyie unyama
huu…nalala nje na mwanangu wa mwezi mmoja “anasema kwa kukata tamaa.

Anadai anapozwa na kutembea na wake za watu.
Anadai tuhuma hiyo nyuma yake ina agenda ya kuwa ana mahusiano na wake
za watu miongoni mwao wakiwemo waliokuwa wakiongoza kundi hilo
kuhakikisha wanawafukuza kijijini hapo,madai aliyosema yapo yenye
ukweli ,lakini walitakiwa kumsubiri wamkamate.

“Wanashindwa kusema tu kuwa natembea na wake za watu ingawa hawajawahi
kunikamata na wamekuwa wakidai watahakikisha wananikomesha,kwa ni I
adhabu iwe kwa mama yangu…kaka na familia yake na wake zangu na
wanangu…Mungu atalipa .”anasema na kukaa kimya.

Mwenyekiti wa kijiji aliwahi kufungiwa ofisini na wananchi.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Daniel Magige aliwahi kufungiwa
ofisini na jamii baada ya kufuatilia wezi huko Tarime na kuwapa
taarifa kuwa aliyeuziwa sola  amemwacha huko baada ya kubaini siyo
yenyewe.

Viongozi wa kijiji na kata wakwepa kulizungumzia.
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho Samweli Makena na ofisa mtendaji wa
kata hiyo Shaweshi Sipemba wamekwepa kuzungumzia sakata hilo kwa madai
kuwa liko ngazi za wilaya.

Wanasiasa hukwepa kuzungumzia matatizo  ya wazee wa mila kupoteza kura.
Viongozi wa kisisa hasa wa kuchaguliwa hukwepa kuchomoza kuzungumzia
ukiukwaji wa Haki za binadamu kwa kuogopa kupoteza kura kwa kuwa
wanawatumia wazee wa mila wakati wa uchaguzi.

Diwani wa kata hiyo ambaye ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo
John Ng’oina alipotafutwa kwa njia ya simu na gazeti hili anashindwa
kukubali ama kukataa kuwepo kwa tukio hilo la ukiukwaji wa haki za
binadamu.

“Niko nje ya wilaya nashindwa namna ya kulizungumzia
hilo,”anasema,hata hivyo Mwananchi Jumapili imebaini kuwa novemba
1,2012 ndiye aliongoza kikao cha baraza la madiwani ikiwemo na kamati
zilizotangulia,kwa hivyo wakati tukio linatokea amekuwepo lakini kwa
hofu ya kupoteza kura ana kwepa  kulizungumzia.

Viongozi wa Ritongo.
Mwenyekiti wa ritongo Bhoke Marwa Nyangere,katibu wake Nyakarare
Chacha na baadhi ya wazee wa mila hawakuweza kupatikana kuzungumzia
tukio ambalo mtuhumiwa anawataja kuwa ndio walioongoza watu
waliotekeleza unyama huo,juhudi zinaendelea za kuwatafuta.

Katibu tawala asema waliohusika wakamatwe.
Katibu tawala wa wilaya hizo Magohu Isenzo amelithibitishia mwananchi
Jumapili kuwa waliohusika watakamatwa kwa kuwa wamevunja sheria na
kukiuka Haki za Binadamu.

“Ritongo si chombo cha kisheria na wanapokuwa wanajambo wanaleta kwetu
sisi barua kabla ya… tukiona wanakiuka haki za binadamu
tunakataa,hawakuleta kwa kuwa maamzi yao hayana ukweli,nimefuatilia
mimi na kamati ya ulinzi na usalama hadi kijiji cha Merenga
waliwashangaa kwa uamzi huo,pia hapakuwa na mtu aliyejitokeza kumtaja
wanayemtuhumu”anasema.

“Tumefika kwenye kikao chao oktoba 27 nikiwa na kamati ya ulinzi na
usalama hapakuwa na aliyejitokeza kumtaja wanayemtuhumu,tukakubaliana
wamjengee nyumba zake kwa kuwa wamemfanyia ukatili kimakosa,wakasema
wataanza na nyumba mbili kisha wanaendelea,baadae wamegoma kuwa
hawatajenga sasa lazima tukamate viongozi wao”anafafanua.

Kuhusu waliouza ardhi ya Sungura amesema wanajidanganya na watapata
hasara walionunua kwa kuwa hakuna utaratibu wa hivyo,na kusisitiza
vyombo vya ulinzi na usalama vitawakamata vinara wa ukatili huo.

Walipanga kumpigia yowe katibu tawala.

Habari za uhakika ambazo Mwananchi Jumapili imezipata na kuthibitishwa
na katibu tawala zinadai kuwa wananchi hao walipanga kumpigia yowe
kama angekwenda kufuatilia tatizo hilo.

Wanaharakati.
Samweli Mewama Mwenyekiti wa shirika la Wasaidizi wa Sheria na Haki za
Binadamu wilayani Serngeti(WASHEHABISE)anasema ukiukwaji wa Haki za
binadamu uliofanywa ni matokeo ya serikali kutumia vyombo visivyo vya
kisheria kutoa maamzi.

“Huo ni mwendelezo wa matukio ya Ukiukwaji wa haki za binadamu
unaofanywa na wazee wa mila na vikao vyao vya
ritongo,tumesema,tumeelimisha lakini wanapata nguvu za
serikali,havitakiwi kuvumiliwa maana vinakiuka katiba ya nchi na
sheria zake za utawala bora”anasema.

Anasema shirika linafuatilia kuhakikisha anapata haki zake na
waliohusika wanakamatwa maana wanavunja katiba ya nchi inayotoa nafasi
ya kumiliki mali,na matendo kama hayo yanayobebwa na wanasiasa wenye
mitizamo hasi kuifanya wilaya na mkoa huo kuonekana unaongoza kwa
matendo ya ukatili,taswira ambayo inaweza kutokomezwa kama mamlaka
zitatimiza wajibu wake.

Mwisho.

0 comments:

Post a Comment