Mjumbe wa Umoja wa Wanaotetea Katiba
ya Wananchi (Ukawa), Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza na waandishi mjini
Dodoma jana, mara baada ya kujadili hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa
katika Bunge Maalumu la Katiba juzi. Kushoto ni Mjumbe wa Ukawa, Freeman Mbowe
na kulia ni Tundu Lissu. Picha na Salim Shao
Na Mussa Juma, Mwananchi
Posted Jumapili,Marchi23 2014 saa 11:17 AM
Posted Jumapili,Marchi23 2014 saa 11:17 AM
Kwa ufupi
Alisema kauli za Rais badala ya
kuimarisha umoja zimewagawa Watanzania kwani ametoa vitisho ambavyo havina
sababu hasa kwa Wapemba bila kujua kuna Wanyamwezi wanaoishi Zanzibar.
Dodoma. Bunge Maalumu la Katiba sasa lipo katika hati hati ya
kuendelea kutokana na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
kutangaza kuwa hawatakuwa tayari kujadili rasimu tofauti na iliyowasilishwa na
Jaji Joseph Warioba bungeni.
Wakizungumza katika mkutano na
waandishi wa habari jana katika Ukumbi wa Pius Msekwa bungeni, viongozi wa
Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, James Mbatia, Freeman Mbowe na Tundu Lissu,
walisema wataitetea rasimu hiyo, ndani ya Bunge na kwenye Kamati.
“Rais Jakaya Kikwete amekuja bungeni
siyo kufungua Bunge la Katiba bali kaja na mapendekezo ya rasimu ya CCM, sisi
tutajadili rasimu ya wananchi ya Jaji Joseph Warioba ambayo inazungumzia muundo
wa Muungano wa Serikali tatu,” alisema Profesa Lipumba.
Kutokana na msimamo huu wa Ukawa
huenda Bunge litakwama kwani kwa mapendekezo ya CCM yenye Muundo wa Muungano wa
Serikali mbili ni lazima kuandikwa upya Rasimu ya Katiba au kufanyika
mabadiliko makubwa.
Profesa Lipumba alisema katika
majadiliano juu ya rasimu, Ukawa watajikita kutumia Rasimu ya Katiba waliyopewa
na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo imeeleza mapendekezo kwa nini
yamefikiwa katika kila hoja,” alisema.
Hata hivyo, alisema wamesikitishwa
sana na Rais Jakaya Kikwete, badala ya kufungua Bunge alijikita katika kuchambua
rasimu na kuikosoa tume aliyoiunda mwenyewe.
“Rais Jakaya Kikwete siyo tu
amemdhalilisha Jaji Warioba pamoja na wajumbe wa Tume, bali amewadhalilisha
wananchi waliotoa maoni kwani hata takwimu alizotoa za kupinga rasimu siyo za
kweli,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema muundo wa Serikali tatu ndio
mawazo ya wananchi ambayo yamekusanywa na watu wenye heshma wakiwapo Jaji
Warioba aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais na Jaji Augustino
Ramadhani ambaye pia amewahi kuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Jaji Mkuu wa Zanzibar.
Alisema kauli za Rais badala ya
kuimarisha umoja zimewagawa Watanzania kwani ametoa vitisho ambavyo havina
sababu hasa kwa Wapemba bila kujua kuna Wanyamwezi wanaoishi Zanzibar.
Mbatia
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James
Mbatia ambaye pia ni mjumbe wa Bunge hilo, alisema kwa kauli ya juzi ya Rais
Kikwete, kutangaza kuwapatia Zanzibar; watu, ardhi, mamlaka kamili na kusimamia
uhusiano wa kimataifa ni kuvunja rasmi Muungano,
Mbatia alisema Rais Kikwete pia
amewagawa Watanzania katika kauli zake ikiwa ni pamoja na ile ya Wapemba kwa
kulima vitunguu katika Jimbo la Kibakwe kana kwamba ni makosa.
Alisema wamesikitishwa na Rais kuacha kufungua Bunge badala yake
katumia taarifa potofu za mitaani kuligawa Bunge na kuwadhalilisha
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Hakuna asiyejua sasa tupo katika mgogoro mkubwa
wa kikatiba, Zanzibar tayari ni nchi kamili kutokana na mabadiliko ya 10
ya katiba yao waliyoyafanya mwaka 2010 baada ya kupitisha dhana ya kuwa
Zanzibar ni nchi,” alisema.
Mbowe
Mbowe alisema Rais amevunja maridhiano na hata
kushindwa kusikiliza maoni ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya,
Seneta Amos Wako kuwa maoni ya wananchi yaheshimiwe.
Alisema Serikali ya Kenya ilichakachua maoni,
ilichakachua rasimu na kusababisha vurugu kubwa jambo ambalo linaweza
kutokea kwa Tanzania.
“CCM wasijidanganye kwa wingi wao bungeni hakika katika hili tutatetea madai na maoni ya wananchi hadi mwisho,” alisema