ASKARI SENAPA WAUA
JANGILI,WAKAMATA BUNDUKI SMG AK 47 ,RISASI 258.
Na Mwandishi
wetu-Serengeti.
Novemba 30,2012.
ASKARI wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti wamefanikiwa kumuua
mtuhumiwa mmoja wa ujangili ,kukamata silaha ya kivita aina ya Smg AK 47,risasi258
, meno mawili ya tembo na msumeno wa kukatia meno ya tembo na shoka.
Tukio limethibitishwa na kamanda wa polisi mkoa wa Mara
Absalom Mwakyoma linadaiwa kutokea novemba 29,majira ya saa 12;30 jioni katika
eneo la Itaro ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti,eneo ambalo kumewekwa Faru
waliotolewa Afrika Kusini,maarufu kama Faru wa JK.
Alisema aliyeuawa hajafamika ingawa anakisiwa kuwa na umri
kati ya miaka 27,33 na kuwa katika majibizano hayo alipigwa risasi mguu wa
kulia iliyopelekea kufa na wenzake wanakisiwa kuwa wanne kukimbia ,na hakuna
aliyekamatwa kutokana na tukio hilo.
Habari za uhakika kutoka eneo la tukio zinadai kuwa askari
wa hifadhi hiyo wakiwa doria walisikia milio ya bunduki na kufuatilia walikuta
kundi kubwa la majangili wanaokadiriwa kufikia watano wakiwa na silaha za kivita wameishaua tembo
mmoja na wametoa meno.
“Walianza kutushambulia kwa risasi,kukatokea majibizano
makali yaliyochukua muda ambayo yanaonyesha kuwa walikuwa na risasi za kutosha kwa
kuwa walikuwa na silaha za kivita,mmoja akawa amepigwa risasi na kuanguka
…wenzake walipoona hivyo wakakimbia mmoja akiwa na bunduki,”kulisema chanzo
kimoja cha uhakika.
“Maiti hiyo imehifadhiwa katika chumba cha maiti hospitali
teule ya Nyerere ddh,haijatambuliwa ,inaonekana si mtu wa maeneo haya hali
ambayo inaonyesha ukubwa wa mtandao huo kutoka mikoa mbalimbali kwa
kushirikiana na wenyeji wa maeneo,kasi yao kuingia inakwenda sambamba na
uingizaji silaha kutoka mikoa iliyoko pembezoni mwa mipaka ya nchi
jilani”kilisema chanzo hicho.
Mganga mkuu wa Hospitali hiyo dk,Kelvin Mwasha amethibitisha
kupokelewa kwa mwili wa marehemu huyo”amefikishwa hapa usiku wa manane na
ameletwa na askari polisi…hawajaja polisi kwa ajili ya uchunguzi,tunawasubiri
maana hatuwezi kusema kilichosababisha kifo bila kufanya uchunguzi”alisema
daktari.
Mtandao wa ujangili ambao umesambaa hifadhi za taifa ,mapori
ya akiba na maeneo ya wazi unadaiwa kufadhiliwa na wafanya biashara wakubwa wa
ndani na nje ya nchi ambao wanahusishwa kuwa na ushirikiano wa karibu na baadhi
ya watendaji wa jeshi la polisi,mahakama,maliasili ,uhamiaji na ofisi za
wanasheria wa serikali na Tra.
Uhusiano huo huwawezesha kusafirisha shehena za meno ya
tembo kwa kupita mipakani,bandarini,na kupeleka nje ya nchi,kasi hiyo ikienda
sambamba na uingizaji wa silaha za kivita kwa ajili ya kazi hiyo.
Wakati huo huo mtu mmoja ambaye hajatambuliwa aliuawa na
wananchi baada ya kukutwa akiiba mabati kwenye jengo la mtu aliyejulikana kwa
jina Jumanne Kagosi katika kijiji cha Kwangwa kata ya Kigera Manispaa ya
Musoma.
Kamanda Mwakyoma amesema tukio hilo limetokea novemba
29,majira ya saa 10 jioni mwaka huu na kuwa wananchi waliamua kuchukua sheria
mkononi na kumpiga hadi kufa ,na kuomba wananchi wasijichukulie sheria mkononi
badala yake wafikishwe kwenye vyombo husika.
Mwisho.