CCM
imemtwisha rasmi Rais Jakaya Kikwete jukumu la kukabiliana na mawaziri ‘mizigo’
wanaoshindwa kutimiza majukumu yao. PICHA | FIDELIS FELIX
Na Fidelis
Butahe, Mwananchi
Posted Jumapili,Decemba15 2013 saa 5:12 AM
Posted Jumapili,Decemba15 2013 saa 5:12 AM
Kwa ufupi
- Mawaziri 7 waliotajwa ni
‘mzigo’ kwa Serikali juzi walihojiwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM
chini ya Mwenyekiti wake Rais Kikwete, ambapo jana Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema wamemshauri Rais Kikwete mambo
matatu; kuwafukuza, kuwahamisha wizara au kuwahimiza wafanye kazi.
Dar es
Salaam. Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kimemtupia mpira Rais Jakaya Kikwete wa kuamua hatima ya
mawaziri saba, wanaotuhumiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Mawaziri
hao waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa Serikali juzi walihojiwa na Kamati Kuu ya
Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais Kikwete, ambapo jana
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema wamemshauri
Rais Kikwete mambo matatu; kuwafukuza, kuwahamisha wizara au kuwahimiza wafanye
kazi.
“Kamati
Kuu imetoa maazimio saba ambayo yote yanazihusu wizara saba zinazoongozwa na
mawaziri hao. Tumemshauri Rais Kikwete, yeye ndiye ataamua nini cha kufanya kwa
sababu ndiye aliyewateuwa mawaziri hao,” alisema Nape.
Wakiwa
Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma katika ziara ya chama hicho, Nape pamoja na
Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana aliwatupia lawama mawaziri hao
wakati wakielezea changamoto zinazowakabili wakulima ambao ni asilimia 80 ya
Watanzania, huku mawaziri husika wakikaa kimya.
Nape
alisema mawaziri hao waliitwa kuhojiwa na kutakiwa kutoa maelezo ya masuala
yaliyoibuliwa wakati wa ziara hiyo ambayo pia iliwahusisha baadhi ya wajumbe wa
Sekretarieti.
Katika
maelezo yake kwa waandishi wa habari jana, Nape aliwataja mawaziri hao kuwa ni
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika Christopher Chiza, Naibu Waziri wa Fedha Saada Mkuya
(alihojiwa kwa niaba ya Waziri wa Fedha Dk William Mgimwa).
Wengine
ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda, Waziri wa Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia.
Sakata la
kutaka mawaziri ‘mizigo’ kutoswa limekuwa likiibuliwa na wabunge mbalimbali
katika mikutano ya Bunge mjini Dodoma, huku baadhi wakipendekeza hata Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda naye atoswe kutokana na kushindwa kuwasimamia mawaziri.
Ushauri
wa CCM kwa JK
Nape
alisema kuwa kazi ya Kamati Kuu ni kushauri, “Kazi yetu ni kushauri na siyo
kufukuza. Rais Kikwete ndiye amewateua mawaziri hao, ameupokea ushauri na yeye
ndiye mwenye uwezo wa kuwafukuza, kuwahamisha au kuwasukuma watende kazi. Hiyo
siyo kazi yetu”
Alipobanwa
zaidi kueleza ushauri ambao Kamati Kuu ilimpa Rais Kikwete Nape alisema, “Kuna
ushauri mwingine ambao tumempa Rais Kikwete hatuwezi kuuweka hadharani.”
Alisema
kuwa wakati wa kuhojiwa kila waziri alikuja na majibu yanayoihusu wizara yake
kutokana na udhaifu ulioelezwa na wananchi.
“Katika
kikao kijacho cha Kamati Kuu moja ya mambo yatakayojadiliwa ni pamoja na
kuangalia utekelezaji wa mambo saba tuliyoishauri Serikali kupitia hizo wizara
saba,” alisema.
Nape
alisema kuwa walipoeleza udhaifu wa mawaziri hao hawakueleza kuwa ni mzigo kwa
Serikali, bali walilenga kueleza upungufu wao katika kusimamia masuala
mbalimbali.
“Mfano
Waziri wa Kilimo kwa miaka minne hajawahi kwenda mkoani Ruvuma ambako kuna
ghala la chakula pia hajawahi kushughulikia matatizo yanayowakabili wakulima wa
korosho na mahindi,” alisema.
Hata
hivyo, Nape alisema kuwafukuza mawaziri siyo dawa na kuweka mambo sawa kwa
maelezo kuwa wakati mwingine utendaji kazi ndani ya Serikali unakwenda ovyo kwa
sababu ya mfumo na sheria mbovu.
“Watu
wanadhani ushauri tuliompa Rais Kikwete ni kuwafukuza mawaziri, wakati mwingine
kufukuza siyo mwisho wa suluhisho. Kwa mfano tumebadili mawaziri Tamisemi
lakini kila mwaka ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) inaonyesha udhaifu katika wizara hiyo,” alisema Nape.
Maagizo
Nape
alisema agizo la kwanza ni kuhusu kilimo cha pamba ambapo Kamati Kuu iangalie
upya Serikali ipitie upya upatikanaji wa pembejeo za ruzuku kwa wakulima wa
pamba nchini.
Alisema
kuwa kuhusu kilimo cha mkataba kwa wakulima wa pamba, Serikali imetakiwa
kuratibu utaratibu wa kilimo hicho ikiwamo kutowalazimisha.
“Kwa
mfano Waziri husika hajafika kwa muda wa miaka minne na nusu mkoani Ruvuma
ambako ndiko kuna ghala la chakula na tulipofika Tunduma tulikuta foleni pale
mizani huku watumishi wakiwa wanafanya kazi kwa saa tisa, lakini baada ya
kueleza udhaifu huo sasa wanafanya kwa saa 24,” alisema.
Aliongeza,
“Chama kimeiagiza serikali kutowalazimisha wakulima kutumia mbegu ya Quiton,
badala yake elimu itumike zaidi badala ya nguvu.”
Alisisitiza
kuwa Kamati Kuu imeitaka Serikali kuangalia upya urasimu katika uwekezaji wa
viwanda nchini, hasa vinavyoongeza thamani ya mazao na kutoa ajira.
Kwa
upande wa wakulima wa korosho, Nape alisema kuwa Kamati Kuu imeisisitizia
serikali kujipanga kutatua tatizo la korosho na kuhakikisha inabanguliwa
nchini.
“Serikali
inatakiwa kuangalia upya orodha ndefu ya makato kwa wakulima hasa wa korosho na
vyama vya msingi au mamlaka zinginezo, ili kuondoa makato yasiyo ya lazima na
kuongeza kipato cha mkulima,”
“Kuhusu
pembejeo za ruzuku Kamati Kuu imepokea taarifa ya malalamiko ya wakulima juu ya
ufanyaji kazi wa mbolea ya Minjingu na kuagiza wananchi wawe huru kutumia
mbolea wanayoitaka badala ya kulazimishwa,” alisema.
Kwa
upande wakulima wa mahindi alisema kuwa serikali imetakiwa kumalizia malipo
yaliyobaki na kuhakikisha wanakomesha utaratibu wa kuwakopa wananchi mazao yao
bila kuwalipa.
“Utaratibu
uwekwe wa kufanya tathmini mapema ya mahitaji na uwezo wa kununua mahindi wa
serikali ili kuepusha utaratibu wa kuchukua mahindi ya wakulima bila
kuwalipa,”alisema.
Nnauye
alisema kwa upande wa madai ya walimu Kamati Kuu imeiagiza Serikali kukamilisha
uhakiki wa madai ya walimu na kuwalipa haki zao ikiwamo kuhakikisha madeni
hayazaliwi tena.
Kamati
hiyo pia imekemea watendaji wachache wanaojihusisha na ubadhirifu kwenye
halmashauri mbalimbali nchini.
“Serikali
imeshauriwa kuangalia upya sheria kama zinakidhi mahitaji ya wakati na
mazingira ya sasa ili kuongeza uwezo wa udhibiti na kuokoa pesa za walipakodi
zinazopotea kwa walafi wachache kwenye halmashauri mbalimbali nchini,” alisema
Nnauye.
Kwa
upande wa matatizo ya upatikanaji wa maji safi na salama serikali imeagizwa
kufanya mkakati wa makusudi na wa dharura kulitafutia ufumbuzi wa haraka na wa
kudumu tatizo hilo ikiwamo kuangalia upya utaratibu uliotumika kuwamilikisha
watu wachache maeneo makubwa ya ardhi, ambao wameshindwa kuyaendeleza badala
yake wanayatumia kuwakodishia wakulima wadogo.