Posted Decemba28 2013 saa 9:28 AM
Na Goodluck Eliona, Mwananchi
Kwa ufupi
- Wanafunzi hao ni kati ya
844,938 waliofanya mtihani wa darasa la saba Septemba 11 na 12, 20013,
ambapo 427,609 walifaulu kwa kupata alama A na C, ambayo ni sawa na
asilimia 50.61 ya ufaulu.
Dar es Salaam. Serikali imetangaza idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato
cha kwanza mwakani, huku 16,482 wakishindwa kuchaguliwa kutokana na uhaba wa
madarasa.
Wanafunzi hao ni kati ya 844,938 waliofanya mtihani wa darasa la saba
Septemba 11 na 12, 20013, ambapo 427,609 walifaulu kwa kupata alama A na C,
ambayo ni sawa na asilimia 50.61 ya ufaulu ikiwa ni ongezeko la asilimia 19
ikilinganishwa na matokeo ya mwaka jana.
Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Ofisi
ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini
alisema jumla ya wanafunzi 867,983 walisajiliwa kufanya mtihani huo, lakini
wanafunzi 23,045 hawakufanya kutokana na utoro, vifo na ugonjwa.
Alisema kuwa kutokana na ongezeko la fursa ya utoaji wa elimu ya
sekondari nchini, wanafunzi 411,127 kati ya 427,609 waliofaulu mtihani
wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za serikali awamu ya
kwanza huku zaidi ya 16,000 wakikosa kuchaguliwa kutokana na uhaba wa vyumba
vya madarasa 412.
“Idadi hiyo ni sawa na asilimia 96.15 ya wanafunzi waliofaulu mtihani.
Kati ya wanafunzi hao wasichana ni 201,021 sawa na asilimia 95.9 na wavulana ni
210,106 sawa na asilimia 96.3,” alisema Sagini na kuongeza kuwa:
“Ninaziagiza Halmashauri zilizobaki katika awamu ya kwanza ya uchaguzi
kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuwawezesha wanafunzi kujiunga na
kidato cha kwanza ifikapo Machi 2013.”
Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa ikilinganishwa na matokeo ya mwaka jana,
idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza imeongozeka kwa
asilimia 31.37.
Alisema kuwa mtihani huo ambao ulifanyika Septemba 11 na 12, mwaka huu,
ulisahihishwa kwa kutumia teknolojia ya kompyuta ‘Optical Mark Reader (OMR)’.
“Mwanafunzi aliyepata alama ya juu kabisa kwa upande wa wavulana alipata
244 kati ya 250 huku msichana akipata 241. Mwaka 2012 alama ya juu ilikuwa
237,” alisema.
Akizungumzia vitendo vya udanganyifu kwenye mtihani huo, Sagini
alibainisha kuwa wanafunzi 13 wamefutiwa matokeo yao, ambayo ni idadi ndogo
ikilinganishwa na watahiniwa 219 waliofutiwa matokeo mwaka 2012.
“Napenda kutoa wito kwa walimu, wazazi na jamii kwa ujumla kujiepusha na
vitendo vya udanganyifu kwani vinatoa taswira mbaya kwa taifa na kuwafanya
watoto wetu wawe tegemezi zaidi kuliko kujituma na kujibidiisha katika masomo,”
alisema.
Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo hakutaja viwango vya ufaulu kwa kila somo
kama ambavyo imezoeleka katika mitihani iliyotangulia wala mkoa uliofanya
vizuri au vibaya. Matokeo ya mwaka huu yanaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi
walioshindwa kufanya mtihani imepungua kwa wanafunzi zaidi ya 6,000
ikilinganishwa na 29,012 ambao hawakufanya mtihani huo mwaka jana.
Huku idadi ya wasichana na wavulana walioshindwa kufanya mtihani
ikipungua kutoka wasichana 12,501 mwaka jana hadi 9,781 mwaka huu na wavulana
16,511 hadi 13,264.
Matokeo hayo yameshindwa kufikiwa kwa malengo ya mpango wa Serikali wa
Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambao uliwataka walimu kuhakikisha kuwa wanapandisha
kiwango cha ufaulu hadi kufikia asilimia 60.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa BRN kwenye sekta ya elimu
jijini Dar es Salaam, Agosti mwaka huu, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Dk Shukuru Kawambwa, alisema kuwa kiwango hicho cha ufaulu kilitakiwa kuanza
kutumika mwaka huu. Aliwapongeza walimu, walimu wakuu, kamati za shule,
waratibu wa Elimu Kata, Viongozi wa Halmashauri na wadau wote wa elimu ambao
wanasimamia na kuendesha utoaji wa elimu nchini.
Akisoma hotuba ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, bungeni Dodoma
mwaka huu, Dk Kawambwa alisema kuwa serikali itafanya ufuatialiaji wa namna ya
uendeshaji wa mitihani ya darasa la nne, mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.
Mitihani mingine aliitaja kuwa ni wa ufundi stadi katika Halmashauri
tisa ambazo ni Temeke, Ilala, Kinondoni, Morogoro Mjini, Morogoro Vijijini,
Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini, Bagamoyo na Kisarawe, ili kubaini wanafunzi
wenye matatizo katika ujifunzaji.