MGOGORO kati ya wakulima na
wafugaji wilayani Kiteto, Manyara umeingia sura mpya baada ya wafugaji wa jamii
ya Kimasai kuwavamia wakulima na kusababisha vifo vya watu wanne.
Taarifa
ya Mkuu wa Polisi Mkoa wa Manyara, Akilimali Mpwapwa, ilieleza kati ya watu
hao, watatu walikufa hapo hapo na mmoja akiwa njiani kupelekwa hospitali ya
rufaa ya Mkoa wa Dodoma na majeruhi saba.
Alisema
usiku wa kuamkia Jumamosi, wafugaji waliingiza mifugo yao katika mashamba ya
wakulima katika eneo la Kijiji cha Olupoponyi, Kitongoji cha Kalakala.
Alisema
kitendo hicho ndicho kilichosababisha wakulima nao kuanza kuwazuia wafugaji na
mifugo yao kutolisha mimea yao, lakini baada ya hapo wafugaji walionekana kuwa
wabishi na kuanza kuwashambulia.
“Kutokana
na majibishano kati ya wafugaji na wakulima ilisababisha wakulima watatu
kupoteza maisha na majeruhi saba ambao walilazwa katika hospitali ya Wilaya ya
Kiteto,” alisema.
Mauaji
hayo yalitokea Kijiji cha Olupoponyi, Kitongoji cha Kalakala ambapo Mbunge wa
Kiteto na Naibu Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Benedict Ole-Nangoro
(CCM) anaishi.
Imeelezwa
jamii ya wafugaji wa Kimasai waliwavamia wakulima wakiwa katika vibanda vyao
wamelala, saa 7 usiku na kuanza kuwashambulia kwa mapanga, sime, mikuki, visu
na risasi.
Mbunge wa
Kongwa na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema kitendo ambacho kinafanywa
na wafugaji dhidi ya wakulima ni cha kinyama zaidi.
Hata
hivyo, alieleza kushangazwa na serikali kufumbia macho mgogoro huo ambao
kimsingi ni wa miaka mingi.
“Wafugaji
wa jamii ya Kimasai wamekuwa wakiwaua wakulima mara kwa mara na wala suala hili
si geni, viongozi wa ngazi ya juu wamekuwa wakiambiwa masuala haya, lakini
kinachoshangaza ni kuona ukimya wa viongozi,” alisema.
Mbali na
hilo, alimshambulia mbunge wa Kiteto, Ole-Nangoro kuwa ni kati ya viongozi wanaochochea
chuki na kukuza ukabila katika Wilaya ya Kiteto.
Hivi
karibuni, Ndugai alifanya mkutano na wakulima katika mji mdogo wa Kibaigwa,
wilayani Kongwa na kuwaeleza kuwa Wilaya ya Kiteto kwa sasa imechafuka kutokana
na viongozi wake kuwa na tabia ya kuendekeza ukabila.
Mbali na
kuwepo na vitendo vya ukabila na ubaguzi, aliwataja Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk.
Rehema Nchimbi na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Elaston Mbwilo kuwa wanahusika
kwa kiasi kikubwa kuchochea mgogoro kutokana na kupokea rushwa kutoka kwa
wafugaji.