Subscribe:

Ads 468x60px

Mawakili wamng`ang`ania Pinda kesi ya Kikatiba


Na Hellen Mwango
12th December 2013


Waziri Mkuu,Mizengo Pinda
Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imeambiwa kwamba kesi ya kikatiba dhidi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ina mashiko ya kisheria na  inastahili kusikilizwa na mahakama hiyo na kutolewa maamuzi.

Kesi hiyo ilifunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Madai hayo yalitolewa jijini Dar es Salaam jana na upande wa walalamikaji kupitia kwa Makamu wa Rais wa TLS, Wakili Peter Kibatala, wakati akijibu hoja za pingamizi la awali la walalamikiwa kwamba kesi hiyo ilifunguliwa kimakosa na haina mashiko ya kisheria na hivyo mahakama iitupilie mbali.

Kibatala aliwasilisha hoja zake mbele ya jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu, akisaidiana na Jaji Augustine Mwarija na Dk. Fauz Twaib.

Upande wa walalamikiwa uliongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu, George Masaju, akisaidiana na Mawakili wa Serikali Wakuu, Gabriel Marata, Sarah Mlipano na Alesia Mbuya.

Wakili Kibatala alidai kuwa hoja za upande wa walalamikiwa kwamba kesi  isisikilizwe kwa madai ni ya kizushi na haina mashiko, hazina ukweli na kwamba inastahili kusikilizwa na kutolewa maamuzi.

"Kesi hii ina mashiko ya kisheria na tuna haki ya kuja mahakamani kusikilizwa hata kama Waziri Mkuu ana kinga lakini imepita ukomo wa kikatiba...walalamikiwa wamethibitisha kwamba ina mashiko na kwa sababu hiyo, Naibu Mwanasheria Mkuu aliomba mahakama kesi hii iendeshwe kwa lugha ya Kiswahili kwa maslahi ya umma," alidai.

Akifafanua zaidi alidai kuwa mahakama inatakiwa iseme kwamba kauli aliyoitoa Waziri Mkuu Pinda kama ni sahihi au la.

Alidai kuwa ili mahakama itoe maamuzi, ni lazima kesi isikilizwe kwa pande zote mbili na siyo itoe amri kwa kusikiliza pingamizi la awali.

Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa leo ambapo upande wa walalamikiwa watatoa hoja zao.

Katika madai ya msingi, LHRC na TLS, wanapinga kauli iliyotolewa na Pinda bungeni, Juni 20, mwaka huu, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo.

Pinda anadaiwa kutoa kauli inayolalamikiwa alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu, aliyetaka kujua msimamo wa serikali na mambo mengine, malalamiko dhidi ya vyombo vya dola katika baadhi ya maeneo kama Mtwara, kuwapiga wananchi.