Na Waandishi
Wetu, Mwananchi
Posted Jumatatu,Decemba23 2013 saa 9:33 AM
Kwa ufupi
- Diwani
wa Nyanungu, wilayani Tarime Mkoa wa Mara, Samson Mang’enyi alisema
operesheni hiyo ilifanywa kwa uonevu na kuwaathiri wananchi wanaoishi
pembezoni mwa Hifadhi ya Serengeti.
Mikoani: Wananchi katika mikoa mbalimbali nchini
wameshangilia kung’olewa kwa mawaziri wanne, yakiwa ni matokeo ya uchunguzi wa
Bunge kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili.
Diwani wa Nyanungu, wilayani Tarime Mkoa wa Mara,
Samson Mang’enyi alisema operesheni hiyo ilifanywa kwa uonevu na kuwaathiri
wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi ya Serengeti.
Mang’enyi alidai kuwa askari wa wanyama pori
wamekuwa wakiwapiga risasi raia na mifugo na kwamba wakati mwingine wamekuwa
wakiwafanyia vitendo vya kinyama kina mama na watoto ambao walikuwa wakiingia
katika Bonde la Nyanungu kuokota kuni.
“Miaka yote hapa kijijini tulikuwa tunategemea
Bonde la Nyanungu katika kulishia mifugo yetu, kulima na kina mama na watoto
kuokota kuni, lakini baada ya kutangazwa Operesheni Tokomeza, kwa kweli hii
nchi haina ubinadamu kwa baadhi ya watu,” alisema diwani huyo.
Mkazi mwingine wa kata hiyo, Caro Chacha alisema
afya yake kwa sasa inazidi kuzorota baada ya kuchapwa viboko visivyo na idadi
na baadhi ya askari wanyama pori wa Hifadhi ya Serengeti (Senapa) alipokuwa
akiokota kuni katika Bonde la Nyanungu.
“Kwa kweli kipigo nilichokipata sitakisahau katika
maisha yangu. Nilikuwa nanyonyesha lakini nilishindwa hata kunyonyesha mtoto,
hata namna ya kujisaidia haja ndogo nilishindwa. Ila Mungu ni mkubwa,” alisema
na kuongeza:
“Askari hao walifikia hatua na kutuvua nguo zote,
tukabakia uchi wa mnyama kama tulivyozaliwa, jamani inauma sana kwani pale
walikuwapo watoto, walitufanyia vitendo vya ajabu sana. Walitaka hata kutubaka
ila walishindwa baada ya kuona tumeishiwa nguvu kwa mateso ya muda mrefu.”
Ruvuma
Mkoani Ruvuma, wananchi wamekuwa na maoni
yanayokinzana, baadhi wamepongeza uamuzi wa Bunge na baadaye Serikali, wakati
wengine wameeleza kusikitishwa.
Mkazi wa Tunduru, Ajiri Omary Kalolo alisema anaunga
mkono uamuzi wa mawaziri kuondolewa madarakani akisema naye ni mmoja wa watu
walioteswa na askari waliohusika na Operesheni Tokomeza Ujangili.
Kalolo alisema mbali na mateso aliyopata, aliwekwa
mahabusu, kunyang’anywa fedha na kushinda njaa.
“Ninaunga mkono kung’olewa mawaziri wenye dhamana.
Hili ni funzo, kwani nchi ingekufumbua macho tatizo hili tungeweza kufika
pabaya zaidi ingawa najua wapo askari ambao wametesa wananchi kwa matakwa yao
na hawakutumwa kufanya hivyo, tunaiomba Serikali iwachukulie hatua zaidi,”
alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa
wa Ruvuma, Andrew Kuchonjoma ambaye pia alikamatwa na kuwekwa mahabusu kwa siku
tatu kwa kosa la kukutwa na mbao, alielezea kusikitishwa kwake na
kung’olewa kwa mawaziri kwa makosa yaliyofanywa na watendaji waliopo chini yao.
Alisema hatua ya mawaziri kung’oka haitoshi
badala yake akataka Serikali iwachukulie hatua askari wote waliofanya vitendo
vya ukatili.
Morogoro
Katika Wilaya za Ulanga na Kilombero mkoani
Morogoro, baadhi ya wananchi wameeleza kufurahishwa kwao na uamuzi wa Serikali
wa kuwawajibisha mawaziri hao wakisema operesheni hiyo ilisababisha vifo vya
watu na wanyama na kwamba hata walipolalamika hawakusikilizwa.
Mmoja wa watu aliyedai kwamba ndugu zake waliuawa
katika operesheni hiyo, Hamis Kewala alisema suala la kumalizika kwa ujangili
linahitaji umakini kwani wahusika walio wengi wamekuwa wakitumia mbinu mpya
kuua tembo na kusafirisha meno hayo, huku wasiohusika wakiumizwa bila hatia.
Mkazi mwingine, Mohamed Nguku alisema: “Vita hii
sasa itakosa nguvu, suala la msingi ni kuhakikisha usimamizi wa hali ya juu na
umakini, halafu taratibu na sheria za nchi kwa wanaopewa dhamana kufanya kazi
hizi lazima zifuatwe na siyo kufanya wanavyojua wao”.
Agosti 12 mwaka huu, Mkazi wa Tarafa ya Mwaya
wilayani Ulanga, January Gunena alikamatwa na kupelekwa katika kambi ya mateso
iliyokuwa katika Hifadhi ya Selous na kuteswa na baadaye alifariki dunia.
Wengine waliopatwa na mateso hayo ni madereva
wanaoendesha magari yanayofanya safari kati ya Ifakara, Mahenge na Mwaya ambao
wakiwa safarini walikuwa wakisimamishwa na askari kuhojiwa lakini wengine
wakiishia kupata vipigo na kuporwa fedha.
Imeandikwa na: Florence Focus (Tarime),
Joyce Joliga (Songea), Lilian Lucas (Morogoro).