Jairo alisimamishwa kazi kutokana na
tuhuma za kuchangisha fedha kinyume cha sheria kwa lengo la kusaidia mchakato
wa kupitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, katika mwaka wa Fedha
2011/2012 .
Na Elias Msuya, Mwananchi
Posted Decemba28 2013 saa 9:11 AM
Posted Decemba28 2013 saa 9:11 AM
Kwa ufupi
- Serikali iliahidi
kuwasilisha taarifa bungeni ya utekelezaji wa maagizo ya Bunge
kuhusu Jairo na wengine, ambayo bado hayajasomwa
- Ikulu yasema hawana hatia,
Ramo Makani ashangaa Bunge halijapata taarifa
Serikali imewasafisha aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, Blandina Nyoni na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
David Jairo huku ikimpandisha cheo aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali Deo
Mtasiwa.
Nyoni alisimamishwa kazi pamoja na aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk
Deo Mtasiwa na wote kwa pamoja walikuwa na tuhuma za kutumia vibaya
madaraka yao wakiwa watumishi wa umma.
Jairo kwa upande wake alisimamishwa kazi kutokana na kuchangisha fedha
kinyume cha sheria kwa lengo la kusaidia mchakato wa kupitisha bajeti ya wizara
yake, katika mwaka wa fedha 2011/2012 na sasa ameondolewa kwenye utumishi wa
umma, huku Bunge likiwa bado halijapata taarifa ya utekelezaji wa maazimio
yanayomuhusu.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Nyoni kwa sasa amerejea kwa
mwajiri wake wa awali, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akishikilia nafasi ya
mmoja wa wakuu wa idara, huku Dk Mtasiwa akiwa ameteuliwa kuwa Naibu Katibu
Mkuu, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa
(Tamisemi).
Katibu Mkuu Kiongozi
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amelithibitishia gazeti
hili kuhusu watumishi hao na kwamba taratibu zimefuatwa.
“Mimi ninachojua ni kwamba Blandina alikuwa mwajiriwa wa TRA na mkataba
wake ulikuwa haujaisha… Siyo kwamba alikuwa na mikataba miwili, kwenye utumishi
wa umma huwa kuna utaratibu wa kuazima watumishi wa umma.
Ndiyo maana unaweza kukuta mwanajeshi anatolewa jeshini na kupelekwa
uraiani au mtumishi kutoka idara moja kwenda nyingine. Kwa upande wetu sisi
tulishamwondoa kwenye ukatibu mkuu na kule TRA hakuwa na tatizo,” alisema
Balozi Sefue.
Kuhusu Dk Mtasiwa alisema: Uteuzi wa Dk Mtasiwa ulikuwa wazi na hata
alipoapishwa mambo yote yalitangazwa hadharani.” Aliendelea kufafanua kuhusu
Jairo akisema: “Jairo alishaondolewa kwenye ukatibu mkuu, siyo mtumishi tena wa
umma.” Naye Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard
Kayombo alimtetea Nyoni akisema kuwa amerudi kwenye ajira yake ya awali.
“Siyo kwamba ameajiriwa TRA, amerudi tu kwenye ajira yake ya zamani,
alikuwa akifanya kazi hapa akaazimwa na sasa amerudi,” alisema Kayombo na
kuongeza: “Kwani amefanya kosa gani? Kuna mashtaka yoyote aliyofanya unaweza
kuyathibitisha?”
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Bodi ya TRA, Bernard Mchomvu
ambaye alisema Nyoni alishasafishwa na Serikali ndiyo maana wamempokea. “Yule
aliazimwa tu na Serikali…Sasa kama Serikali imesham-clear sisi tutamkataaje?”
alihoji na kuongeza:
“Kwa sababu sikumwomba huyo mtu, nimeambiwa kwamba huyo yuko safi mimi
nifanyeje? Unajua watu wanafurahia wengine wakipata matatizo, hata kama mtu
ameua, basi walete ushahidi. Hata unaposema nchi imejaa rushwa, ulete ushahidi…
kama Serikali imeshamsafisha, ningemkataa ningekuwa mtu wa ajabu.”
Jitihada za kumpata Nyoni
kupitia simu yake ya mkononi hazikuzaa matunda, baada ya simu yake kupokelewa
na sauti ya kiume iliyosema kuwa namba imekosewa.Hata alipotafutwa kwa namba nyingine, simu ilipokelewa na mwanamke aliyejitambulisha kama mfanyakazi wa Wizara ya Afya na kwamba namba hiyo kwa sasa haitumii tena. Alipotafutwa kwa njia ya simu, Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashilillah, alisema suala hilo aulizwe msemaji wa Serikali juu ya Bunge.
“Ongea na msemaji wa Serikali juu ya mambo ya Bunge,” alijibu kwa njia ya ujumbe wa simu.
Lukuvi
Naye Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Bunge, William Lukuvi alisema kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa hayuko ofisini.
“Niko ‘airport’ nasafiri kwenda South Africa, msinipigie simu, siko ofisini hadi mwezi ujao (Januari),” alisema Lukuvi na kukata simu yake.
Awali alipoulizwa kwa njia ya simu baada ya mwandishi kuelezea suala hilo alisema ana kazi nyingi na kwamba apigiwe baadaye.
Makani azungumza
Mwenye wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza tuhuma hizo, Ramo Makani, ambaye pia ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini, akizungumza na gazeti hili kuwa: “Ni kweli mimi nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge iliyochunguza suala hilo, kwa utaratibu kamati kama hiyo huundwa kwa kanuni za Bunge kwa kupewa majukumu maalumu… Kama mbunge tu ningefurahi kusikia taarifa ya Serikali bungeni baada ya kupata taarifa ya Bunge,” alisema Makani na kuongeza:
“Serikali iliahidi kuleta taarifa bungeni ya utekelezaji wa maagizo ya Bunge. Mimi sikumbuki kama taarifa hiyo imeshasomwa bungeni, labda wewe mwenzangu umebahatika kuisikia. Kwa hiyo bado tunasubiri… Kama Serikali imechukua hatua, mimi sijui.”
Tuhuma za Nyoni
Nyoni alituhumiwa kutenda makosa saba ambayo yaliainishwa wakati wa mgomo wa madaktari ulioanza Januari mwaka jana, hali iliyomlazimisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kutangaza kumsimamisha kazi ili uchunguzi uweze kufanyika.
Baadhi ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili ni pamoja na kujilipa mshahara wa ziada kupitia Mradi wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP) nje ya mshahara aliokuwa akilipwa na Serikali, kutengua utaratibu rasmi wa kila Idara ya Wizara ya Afya kuwa na ofisa ununuzi wake kwa kujiweka yeye mwenyewe.
Tuhuma nyingine zilikuwa kulazimisha Wizara ya Afya kununua sare za madereva, suti za sikukuu (Sabasaba na Nanenane) na maua kutoka Mariedo bila kushindanisha na muuzaji mwingine kinyume na kanuni za ununuzi.
Katika mikutano yote inayofanyika wizarani, alikuwa akilazimisha Kampuni ya Kaliula Catering Services kupewa zabuni ya kutoa huduma ya chakula kwa washiriki tangu alipotua wizarani kama Katibu Mkuu.
Sakata la Jairo
Hatua ya kumwondoa Jairo katika utumishi wa umma nayo imefanyika kimyakimya kwani Serikali hadi sasa haijawasilisha bungeni majibu ya maazimio ya Bunge kuhusu sakata hilo ambalo pia liliwagusa watumishi wengine wa Wizara ya Nishati na Madini. Maazimio hayo ni yale yaliyotokana na matokeo ya uchunguzi wa Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Makani na kubainisha kuwapo kwa makosa ya kiutumishi na kijinai ambayo yangewafikisha baadhi ya watumishi hao katika vyombo vya sheria.
Mbali na Jairo, kamati hiyo ilipendekeza kuwajibishwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.
Hata hivyo, ni Jairo pekee kati ya hao aliyewajibishwa kwa kusimamishwa kazi na baadaye kuondolewa katika wadhifa wake. Luhanjo alistaafu utumishi wa umma bila kuchukuliwa hatua zozote wakati Utouh anaendelea na wadhifa wake.
Pia katika taarifa yake, Kamati Teule ilisema utaratibu wa uchangishaji wa fedha Sh418.081 milioni uliofanyika katika Wizara ya Nishati na Madini haukuwa na uhalali kwa mujibu wa Katiba, Sheria na Kanuni za Fedha za Umma.
Pamoja na mambo mengine, Bunge liliazimia kwamba ufanyike ukaguzi wa kiuchunguzi (forensic audit) kwa matumizi ya Sh214 milioni, ambazo kati ya hizo Sh126 milioni Kamati Teule ilikataa maelezo ya matumizi yake na Sh88 milioni ni zile zinaotajwa kwamba zilitumika katika kugharimia semina kwa wabunge.
Azimio jingine ni lile lililoitaka Serikali iviagize vyombo vya dola kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma za kughushi na ubadhirifu zilizoelezwa ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kama ilivyoelekezwa.
Baada ya kufikiwa kwa maazimio hayo, Serikali kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe iliahidi kuyafanyia kazi na kuwasilisha majibu bungeni.
“Kwa sababu ya ukubwa na uzito wa taarifa hii, ni vigumu kuitolea majibu yote hapa hapa, ninachoweza kufanya ni kuipokea pia tutakapokuja katika Mkutano wa Sita, tunatarajia kuleta majibu ya hoja zilizomo kwenye taarifa hii,” alisema Chakawe ambaye sasa ni Waziri wa Katiba na Sheria.