Na Daniel
Mjema, Mwananchi
Posted Jumatatu,Decemba23 2013 saa 9:29 AM
Kwa ufupi
- “Kwangu mimi sifa kubwa
zaidi ni kwa Kinana... itakuwa upuuzi chama kinachotawala kikaacha haki
yake ya kuwatetea wanyonge kwa kupima utendaji wa wale kiliowapa dhamana
ya uongozi,” Kisumo
Moshi. Mwanasiasa mkongwe, Peter Kisumo
amesema kuna tatizo katika uchujaji (vetting) wa watu wanaoteuliwa kushika
madaraka ya umma wakiwamo mawaziri na kutaka mfumo huo urekebishwe.
Pia
Kisumo alisema Rais Jakaya Kikwete anapaswa kuiga mfano wa marais
waliomtangulia kwa kuchukua hatua za kuwaondoa mawaziri wanaochafua taswira ya
nchi badala ya kusubiri Bunge.
Akizungumza
jana, Kisumo alisema ni lazima uchujaji wa watu wanaoteuliwa kuwa mawaziri na
watumishi wengine wa ngazi za juu uzingatie uadilifu na siyo mapenzi ya Rais
pekee.
Kisumo
alikuwa akizungumzia hatua ya Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri
wanne iliyotangazwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda baada ya shinikizo kubwa
kutoka kwa wabunge.
Kisumo
alisema ni lazima vyombo vya kumshauri Rais vifanye kazi yake kwa masilahi ya
nchi vinginevyo Watanzania wataendelea kushuhudia mawaziri waking’oka kwa
kushindwa kuwajibika.
Alitolea
mfano kuwa Rais wa Kwanza Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kumteua Chediel
Mgonja (marehemu) kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga lakini akamwondoa kabla ya
kumwidhinisha.
Kisumo
alisema wakati wa Nyerere na hata awamu ya Benjamin Mkapa (1995-2005), wapo
mawaziri waliowajibishwa na Rais lakini awamu zote mbili za Rais Kikwete mambo
yako tofauti.
“Wakati
wa Nyerere akipata taarifa kuwa taswira ya nchi inaharibika alikuwa anawaita na
kuwataka wamuandikie barua ya kujiuzulu lakini awamu zote hizi za Kikwete mambo
yanaanzia bungeni,” alisema na kuongeza:
“Kusubiri
hadi upate shinikizo la Bunge wakati una uwezo wa kuwaondoa watu wako mapema
haipendezi sana… haya nayaona awamu ya Kikwete.”
Mwanasiasa
huyo alimpongeza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwa kufanya kazi ya
kutathmini utendaji wa Serikali akisema hajawahi kupatikana katibu mkuu wa aina
yake tangu 1995.
“Kwangu
mimi sifa kubwa zaidi ni kwa Kinana... itakuwa upuuzi chama kinachotawala
kikaacha haki yake ya kuwatetea wanyonge kwa kupima utendaji wa wale kiliowapa
dhamana ya uongozi,” alisema.