Na
Jacqueline Massano
22nd
December 2013
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda
Watumishi
866 wa serikali wamechukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria kwa ubadhirifu wa
fedha katika halmashauri mbalimbali nchini.
Kauli
hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa akisoma
hotuba ya kuahirisha shughuli za Mkutano wa 14 wa Bunge lililofanyika mjini
hapa.
Pinda
alisema watumishi waliohusika na ubadhirifu wa mali na fedha za Umma
wamechukuliwa hatua mbalimbali zikiwemo kusimamishwa kazi, kushushwa vyeo na kufikishwa
mahakamani.
Aidha,
alisema kesi za watumishi hao ziko katika mahakama na katika vyombo vya nidhamu
vya Halmashauri na Tume ya Utumishi wa Umma kulingana na makosa yao.
Alisema
kutokana na hali hiyo, kati ya mwaka 2011/12 hadi Septemba, mwaka huu jumla ya
wakurugenzi 52, wakuu wa idara 65 na watumishi wengine 746 wamechukuliwa hatua
za kinidhamu na kisheria kwa ubadhirifu wa fedha katika halmashauri mbalimbali
nchini.
“Waliofukuzwa
kazi ni 232, waliosimamishwa 186, waliovuliwa madaraka 33, waliopunguziwa
mshahara 1, walioshushwa cheo 32, walipewa onyo 113, waliofikishwa mahakamani
233 na waliofikishwa polisi na Takukuru 36.
“Serikali
itaendelea kuhimiza nidhamu katika matumizi ya kifedha na vilevile itaendelea
kuchukua hatua dhidi ya watumishi wote watakaokuwa wabadhirifu,” alisema.
Aidha,
alisema pamoja na hatua za kisheria zinazochukuliwa kwa watumishi hao mmoja
mmoja, serikali imeendelea kuchukua hatua nyingine mbalimbali kukabiliana na
tatizo la ubadhirifu wa mali za umma katika halmashauri.
Pinda
alizitaja hatua za kukabiliana na ubadhirifu huo kuwa ni kuongeza uwezo kwa
kuajiri wahasibu wa kutosha katika halmashauri, kuanzisha kamati za mapato na
matumizi katika ngazi zote za halmashauri na kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa
kamati za mapato na matumizi za halmashauri zote.
Alitaja
mbinu nyingine zinazotumika ni kufanya ukaguzi maalum kubaini ufisadi na
ubadhirifu wowote uliojitokeza.
“Kwa
mfano katika mwaka wa fedha 2011/12 kumefanyika ukaguzi maalum kwenye Mamlaka
za Serikali za Mitaa 14 ambazo ni Kilindi, Kiteto, Muheza, Ruangwa, Musoma,
Kilwa, Temeke, Singida, Arusha, Mvomero, Morogoro, Dodoma, Mbarali na Bunda,”
alisema.
Pinda
aliahirisha Bunge hilo hadi Mei 6 mwakani katika mkutano wa 15 wa bajeti.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI